Wakati hali ikiendelea kuwa tete nchini Kenya kumeibuka maswali juu ya kutoonekana kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga katika maandamano ya awamu ya tatu ya siku tatu yalioanza tangu siku ya jumatano.
Kiongozi huyo amejitokeza na kusema kwamba anaugua mafua makali ambayo yalimpata mwanzoni mwa wiki ya maandamano ya kupinga serikali.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha NTV kwa njia ya simu Raila Odinga alisema hata hivyo anaendelea vyema na kuongeza kuwa kutoonekana kwake na kutoshiriki kwa viongozi wengine wakuu wa upinzani katika maandamano hayo kunamanisha ni maandamano ya Wakenya na si viongozi wa upinzani.
”Maandamano sio ya Baba, sio ya Martha au ya Kalonzo au ya mtu mwingine, maandamano ni ya Wakenya wote’’, alisema Odinga.
Maandamano hayo yameitishwa na upinzani kupinga gharama ya juu ya Maisha na na kupinga mswada wa fedha wa 2023 uliozuiwa na mahakama baada ya bunge kuunga mkono.
Aidha Rais William Ruto amesema kwamba serikali yake itaendelea kulinda usalama na demokrasi ya taifa la Kenya kwa hali na mali.