BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limetoa elimu ya matumizi salama ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo na wasambazaji wa mgodi wa Mwakitolyo.
Lengo la mafunzo hayo ni kupunguza madhara ya kemikali hiyo kiafya na kwenye mazingira, kwa jamii inayozunguka mgodi huo kwenye Kata ya Mwakitolyo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Aidha, NEMC kwa kushirikiana na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), wanatekeleza mradi wa kudhibiti matumizi ya Zebaki (EHPMP).
Mradi huo unaotekelezwa Mikoa ya Geita, Mbeya, Singida, Mwanza, Mara, Songwe na Shinyanga kwa Ufadhili wa Benki ya Dunia.
Akiendesha mafunzo hayo Afisa Ufuatiliaji na Tathimini wa mradi huo kutoka NEMC, Hassan Maalim amesema, lengo kuu la utekelezaji wake ni kuwa na mazingira yenye viwango vinavyokubalika vya zebaki kwa mujibu wa mkataba wa Minamata kuhakikisha matumizi ya Zebaki yanadhibitiwa.
Amesema, wachimbaji wengi wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi bila tahadhari wakati wa kuchakata dhahabu, na wengi hawavai gloves mikononi kwa kuhofia dhahabu kubaki bila kujua wanahatarisha usalama wa maisha yao, na kuwakumbusha kuchukua tahadhari.
Na Meneja wa Ukaguzi na Usajili kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa serikali Bi. Magdalena Mtenga, amebainisha kuwa baadhi ya madhara yanayowapata wachimbaji wasipochukua tahadhari, ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa fahamu, figo kuathirika na kuchanganyikiwa kiakili.
Madhara mengine ni kupoteza kumbukumbu, kuwa na msongo wa mawazo muda wote, kupoteza uwezo wa macho kuona vema, mikono kutetemeka, kupunguza nguvu za kiume, kuharibika kwa mimba na watoto kuzaliwa na utindio wa ubongo.
Bi. Mtenga amewataka wwadau hao kujenga tabia ya kufanya vipimo mara kwa mara, ili kujua viwango vya zebaki mwilini mwao na pale vitakapozidi wafuate ushauri wa madaktari watakaopewa.
Mmoja wa wachimbaji walioshiriki mafuzo hayo, Juma Daudi amesema kuwa, hakuwa anajua kama zebaki inaweza kusababisha mimba kuharibika na kupoteza uwezo wa kuona.
Na amekuja kuthibitisha hilo baada ya kumuona mmoja wao ameathirika na zebaki, na kuwa na rangi mbili mwilini mwake na kuahidi kuchukua tahadhari muda wote awapo kazini.