Umoja wa Afrika (AU) umeridhia kumuunga mkono Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson kuwa mgombea pekee kutoka bara la Afrika wa nafasi ya Urais wa Umoja wa Jumuiya ya Mabunge Duniani (Inter-Parliamentary Union-IPU).
Uamuzi huo umefikiwa katika Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika uliofanyika jijini Nairobi, Kenya Julai 13 na 14, 2023 baada ya baraza hilo kupokea na kuridhia ombi la Serikali ya Tanzania la kumuunga mkono Dkt. Tulia katika kugombea nafasi hiyo.
Spika, Dkt. Tulia tayari ameungwa mkono na Bunge la Afrika (PAP), Jukwaa la Maspika wa Mabunge ya Afrika Mashariki (Bureau of Speakers) na Jukwaa la Mabunge ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC PF) katika kugombea nafasi ya urais wa umoja huo.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Oktoba 27, mwaka huu jijini Luanda, nchini Angola.