Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa siku saba kwa wananchi kusalimisha mavazi ya jeshi au yanayofanania na sare za jeshi kuanzia leo Agosti 24, 2023.
Katika taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya Habari, JWTZ imesema baada ya siku saba zilizotolewa kupita, atakayekutwa na mavazi hayo atachukuliwa hatua.
“Zipo baadhi ya taasisi zinazowashonea watumishi wake sare za aina hiyo. Wapo pia wafanyabiashara wanaoingiza nchini mavazi ya aina hiyo na kuyauza kwa baadhi ya raia katika maduka au maeneo yao ya biashara. Wapo baadhi ya wasanii wanaovaa mavazi hayo na kuyatumia wawapo kwenye majukwaa ya kazi zao bila kufuata utaratibu,” amesema.
Aidha, amesema baadhi ya watu wanatumia mavazi hayo kuwatapeli wananchi na wengine kufanya vitendo viovu huku wakidhaniwa kuwa ni wanajeshi kitendo ambacho kimetajwa kuwa ni kinyume na sheria za nchi na kwamba havipaswi kufumbiwa macho.