Watu 13 wanahofiwa kufariki dunia huku wengine 14 wakiokolewa baada ya mitumbwi miwili kuzama ndani ya Ziwa Victoria wakati wakitoka kusali ibada ya Jumapili Kijiji cha Ichigondo Wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt Vicent Naano amesema tukio hilo lilitokea jana saa 12:30 jioni na tayari mwili wa mtoto anayekadiriwa kuwa na mwaka mmoja umeopolewa.
“Watu hawa walikuwa wakitoka kusali katika kanisa la KTMK ndipo mtumbwi mmoja ukapigwa na dhoruba na kuanza kuzama, ukaja mtumbwi wa pili kwaajili ya kuokoa nao ukapigwa na dhoruba mitumbwi yote miwili ikazama,”amesema Dkt Naano
Dkt Naano amesema jitihada za kuwatafuta watu hao 13 zinaendelea akidai jana baada ya giza kuingia zoezi la kuwatafuta lilisitishwa.
“Tupo hapa na timu ya usalama ya wilaya tunaendelea kuwatafuta maana jana baada ya giza kuingia hakuna ambacho kingeweza kufanyika ila tu hadi sasa ni mwili mmoja ndio umeopolewa,” amesema