Mamlaka nchini Iran imetangaza kampeni mpya ya kuwakamata wanawake wasiovaa hijabu, huku polisi wa maadili wakielekezwa kuanza doria kutekeleza sheria za lazima za kuvaa hijab.
Saeid Montazeralmahdi, msemaji wa kikosi cha kutekeleza sheria cha Iran, alithibitisha kwamba doria za polisi sasa zinafanya kazi kwa miguu na kwa magari ili kukabiliana na watu ambao mavazi yao hayaonekani kuwa yanafaa katika Jamhuri ya Kiislamu.
Montazeralmahdi alisema polisi wanatarajia kila mtu kufuata kanuni za mavazi zinazokubalika ili maafisa wawe na muda zaidi wa kushughulikia misheni nyingine muhimu za polisi.
Wanawake wanaofikiriwa kukiuka sheria wanaweza kukamatwa na kupelekwa kwenye kile kinachoitwa vituo vya elimu upya vinavyoendeshwa na polisi kwa ajili ya kupatiwa elimu zaidi ya namna gani wanapaswa kujistiri.