Meneja Maendeleo na Biashara wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Mhandisi Magoti Mtani amesema kuwa hali ya upatikanaji umeme kwa sasa inaelekea kuzuri zaidi ukilinganisha na kipindi kilichopita cha shirika hilo.
Mtani ameyasema hayo leo Machi 27, 2023 mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye kilele cha Wiki ya Kurasa 365 za Mama na kusema kuwa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP) ujenzi wake umefikia asilimia zaidi ya 93 na pindi likikamilika Megawati 2115 zinategemewa kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.
Amesema mradi wa Gesi wa Kinyerezi 1 Extension una uwezo wa kuingiza Megawati 180, lakini mwaka huu tayari imeingiza Megawati 160 huku mradi wa Maporomoko ya maji Rusumo unaolisha nchi ya Tanzania, Rwanda na Burundi tayari unalisha Megawati 27 kwenye gridi yetu ya taifa.