Serikali ya Kagamenchini Rwanda yaamua kufanya mageuzi ya kinishati ukanda wa Afrika Mashariki.
Serikali hiyo ya Kagame imeingia makubaliano ya kutengeneza kinu cha Nyuklia cha majaribio.
Rwanda imeingia makubaliano na Kampuni ya Dual Fluid energy Inc, ya ushirikiano baina ya Kanada na Ujerumani.
Mamlaka ya udhibiti wa Atomiki Rwanda imesema kuwa “Kinu hicho kitatengenezwa kwa teknolojia ya kisasa Zaidi, huku ikitumia nishati ya kimiminika “liquid” na kipoozeo cha madini ya risasi ili kupunguza taka za mionzi hatari”.
Kwa sasa Rwanda ina kinu cha kuzalisha umeme kwa asilimia kubwa kutokana na maji. Na kiasi kingine kinatokana na nshati nyingine kama gesi, Nishati ya jua na nishati nyinginezo.
Hata hivyo inatazamiwa kuwa, hadi kufikia mwaka 2026 ujenzi wa kinu cha majaribio utakuwa umekamilika.
Na majaribio yanatarajiwa kuchukua miaka miwili kuanzia mwaka 2026 hadi 2028.
Majaribio hayo yanatarajiwa kugharimu Zaidi ya Dola milioni 75 za Marekani, na itagaharmiwa na kampuni hiyo, alisema Mtendaji Mkuu wa Dual Fluid Bw. Goetz Ruprecht.
Kinu hicho kinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kuzalisha umeme nchini Rwanda.
Kwa hatua hii ya Rwanda, itakuwa ni nchi ya pili kuzalisha umeme kwa nishati ya nyuklia barani Afrika ikiwa mpango huu utafanikiwa.
Huku nchi ya kwanza ikiwa ni Afrika Kusini, ambayo ilitengenezewa kinu chake na kampuni ya Rosatom.
Kampuni ya Rosatom inamilikiwa na serikali ya Urusi, na inahusika na nishati mbalimbali ikiwemo nyuklia na nishati mbadala.
Huku Uganda kutokana na mipango yake iliyowekwa wazi mwezi Machi mwaka huu, inaweza kuwa ya tatu kuzalisha Umeme kwa kutumia Nyuklia kuanzia mwaka 2031 kama inavyotarajia.
Hata hivyo uzalishaji wa umeme kwa nyuklia ni teknolojia inayolindwa na kuzuiwa mno duniani.
Sababu kuu ikiwa ni uwezekano kuzalisha silaha za maangamizi (Nyuklia) ikiwa teknolojia hiyo itatumika vibaya.