Microsoft italipa dola milioni 20 sawa na Tsh Bilioni 47 kwa mamlaka ya udhibiti wa biashara nchini Marekani baada ya kubainika kuwa imekusanya data isyo halali kuhusu watoto ambao walikuwa wameanzisha akaunti za Xbox.
Tume ya Biashara ya Shirikisho (Federal Trade Commission) imedai kuwa kuanzia 2015 hadi 2020, Microsoft ilikusanya taarifa binafsi za watoto wa chini ya miaka 13 ambao walijiandikisha kwenye mfumo wao wa michezo ya kompyuta ya Xbox bila idhini ya wazazi wao na kuendelea kuwa na taarifa hizo.
FTC imesema Microsoft ilikiuka Sheria ya Ulinzi wa Faragha Mtandaoni kwa Watoto, au (COPPA), hivyo Kampuni hiyo italazimika kuchukua hatua kadhaa za kuimarisha ulinzi wa faragha kwa watumiaji watoto wa mfumo wake wa Xbox.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo, watoa huduma za mtandaoni na tovuti zilizolenga watoto walio chini ya miaka 13 ni lazima ziwajulishe Wazazi kuhusu taarifa za kibinafsi wanazokusanya kutoka kwa Watoto na kupata ridhaa yao ili kukusanya na kutumia taarifa hizo.