Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Sydney (UTS) nchini Australia wamekuja na teknolojia inayotumia sensa (sensor) ambayo inaruhusu kuongoza roboti au kompyuta kwa njia ya mawazo.
Kompyuta hizo zinazoendeshwa kwa kutumia mawazo ya namna mtu anavyofikiri, zimeundwa na watafiti kutoka Jeshi na Kituo cha Ubunifu cha Ulinzi nchini Australia, chini ya usimamizi wa Profesa ChinTeng Lin na Francesca Lacopi kutoka chuo cha Teknolojia Sydney.
Mbali na matumizi ya kijeshi, teknolojia hiyo inatumika pia katika kutengeneza vifaa vya huduma za kiafya kama vile vya kumsaidia mtu mwenye ulemavu kuendesha kiti mwendo (wheelchair) na kiungo bandia (mguu au mkono).
Ubunifu huo umefanikishwa kupitia mbinu ambayo madaktari hutumia kufuatilia mawimbi ya umeme kutoka kwenye ubongo wa binadamu kwa kupandikiza au kuweka kifaa maalum kichwani.
Mbinu hiyo haisaidii tu katika kutambua matatizo ya mfumo wa neva, lakini pia inaweza kutumika kama mashine ya ubongo ambayo hutumia mawimbi ya ubongo kuendesha kifaa kilichopo nje ya mwili kama vile kiungo bandia, roboti au michezo ya video (game).
Profesa Chin Teng Lin na Francesca Lacopi kwa kushirikiana na wenzao wameazimia kutengeneza sensa (sensor) ambayo inaweza kufuatilia kwa usahihi shughuli za ubongo na kuzitafsiri.
Hata hivyo watafiti hao wanaamini kuwa utafiti wao ni hatua ya kwanza kuelekea kujenga vitambuzi vikavu vilivyo imara zaidi, vitakavyotumika kwa urahisi na kupanua matumizi ya miingiliano ya mashine ya ubongo.
Utafiti kamili kuhusu teknolojia hiyo umechapishwa katika jarida la ACS ‘Applied Nano Materials’.