Mahakama ya Kimataifa ya Haki(ICJ) ilisikiliza utetezi wa Israeli dhidi ya tuhuma za Afrika Kusini kwamba ilifanya vitendo vya mauaji ya halaiki huko Gaza, siku ya pili ya kusikilizwa ambayo ilikuwa inaonyeshwa mubashara ulimwenguni kote.
Karibu watu 24,000 wameuawa katika eneo hilo tangu Oktoba 7, karibu 10,000 kati yao ni watoto. Maelfu zaidi wamepotea chini ya vifusi na wanahofiwa kuwa wamekufa.
Afrika Kusini inadai kwamba Israeli imevunja Mkataba wa Mauaji ya Halaiki wa mwaka 1948 katika vita vyake dhidi ya Gaza. Alhamisi, timu ya kisheria inayowakilisha Afrika Kusini iliomba mahakama itoe hatua za dharura kusitisha mashambulizi ya angani yanayoendelea na uvamizi wa ardhi wa eneo hilo.
Ombi hilo la hatua za muda lilikuwa ndio kiini cha kusikilizwa kwa wiki hii.
Katika utetezi wao siku ya Ijumaa, wawakilishi wa Israeli, wakiongozwa na mwanasheria na mwanazuoni wa Uingereza Malcolm Shaw KC, walisema kwamba ombi la Afrika Kusini “limepotosha” na “limeondoa muktadha” wa hatua za kijeshi za Tel Aviv huko Gaza, na kwamba kwa kuishutumu Israeli kwa mauaji ya halaiki, Pretoria ilikuwa “inapunguza” maana ya uhalifu huo.
Hizi hapa ni hoja kuu za kujibu za Israeli na angalia ikiwa zina mashiko:
Haki ya kujilinda
Israeli ilidai kwamba shambulio la Hamas kwenye vituo vya jeshi na vijiji jirani kusini mwa Israeli – pamoja na kuchukua mamia ya mateka – mnamo Oktoba 7 ndio lililoanzisha vita vya Gaza, na kwamba Israeli ina haki ya kujilinda chini ya sheria ya kimataifa.
Tal Becker, mwanasheria wa timu ya Israeli, aliiambia mahakama kwamba Mkataba wa Mauaji ya Halaiki ulitungwa baada ya mauaji ya kimbari ya Wayahudi katika Holocaust na kwamba neno “kamwe tena” ni moja ya “majukumu ya juu zaidi ya kimaadili” kwa Israeli.
Kwa kuomba amri ya muda dhidi ya uvamizi wa Israel, Becker alisema, Afrika Kusini inajaribu kumnyima Israel fursa ya kutimiza majukumu yake kwa wafungwa waliochukuliwa na Waisraeli waliotimuliwa baada ya mashambulizi ya Oktoba 7 kutoka jamii karibu na mpaka wa Gaza.
Lakini Neil Sammonds, mwanaharakati mkuu wa Palestina katika shirika la haki za binadamu la War on Want, aliiambia Al Jazeera kuwa hoja za Israel ni “dhaifu”.
“Bila shaka, Afrika Kusini na mashirika ya haki za binadamu kama sisi wanalaani mauaji ya raia na utekaji nyara [na Hamas],” Sammonds alisema. “Lakini hii haihalalishi majibu ya kutoka kwa Israeli. Kama nguvu inayokalia ardhi, Israel hana haki ya kujilinda – hoja hii haikubaliki.”
ICJ iliamua mwaka wa 2003 kwamba mamlaka inayokalia ardhi kwa nguvu haiwezi kudai haki ya kujilinda, katika kesi iliyohusisha ujenzi wa ukuta wa kugawa katika Ukingo wa Magharibi(West Bank) uliokaliwa na Israel. Israel haijioni kama nchi inayokalia kwa mabavu tangu ilipojiondoa Gaza mwaka 2006. UN na aina mbalimbali ya mashirika ya haki za binadamu wamekataa madai haya, hata hivyo, wakati wasomi wa sheria za kimataifa wamegawanyika kuhusu iwapo Gaza ilikuwa “inayokaliwa kwa nguvu” kulingana na sheria za kimataifa.
Nia ya mauaji ya kimbari
Timu ya wanasheria wa Israel ilisema shutuma za Afrika Kusini kwamba Tel Aviv ina nia ya asili ya “kuwaangamiza” watu wa Palestina zinatokana na “madai ya nasibu”.
Hata hivyo, Akshaya Kumar, mkurugenzi wa utetezi wa migogoro na miradi maalum katika Human Rights Watch, aliiambia Al Jazeera kwamba haikuwezekana kupitisha maoni ya maafisa wa ngazi za juu kama “madai ya nasibu”.
“Baadhi ya taarifa zilizofunua na kubainisha zaidi zilitolewa na rais, waziri mkuu, na waziri wa ulinzi na watunga maamuzi wengine muhimu,” Kumar alisema.
Katika wasilisho lake, Shaw alisema kwamba kauli zilizotolewa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na kutaja “Amalek” – ambayo ilitajwa mahsusi na timu ya Afrika Kusini siku ya Alhamisi – zimetolewa nje ya muktadha.
Katika taarifa iliyotajwa, Netanyahu aliwaambia wanajeshi wa Israel waliokuwa tayari kuvamia Gaza mnamo Oktoba 28 kumbuka “kile Amaleki walichokufanyia”, akirejelea wito wa kibiblia wa kufuta kabisa kikundi maalum cha watu.
Hata hivyo, Shaw alisema kwamba Netanyahu aliendelea kumaliza taarifa kwa kusema “jeshi [la Israel] ni jeshi lenye maadili zaidi … na hufanya kila kitu kuepuka” kuua wasio na hatia.
Katika video zilizopo za rekodi hiyo, Netanyahu hatamki maneno hayo baada ya kurejea hadithi ya Biblia. Alisema, “Wanajeshi na wapiganaji wetu shujaa ambao sasa wako Gaza … na maeneo mengine ya Israel wanajiunga na mnyororo huu wa mashujaa wa Kiyahudi, mnyororo ambao umeanza miaka 3,000 iliyopita kutoka kwa Yoshua ben Nun hadi mashujaa wa 1948 … Wana lengo moja kuu, kushinda kabisa adui muuaji na kuhakikisha uwepo wetu katika nchi hii.”
Vitendo vya mauaji ya kimbari
Katika kujibu madai ya vitendo halisi vya mauaji ya halaiki, yakiwemo mauaji ya halaiki na ya kiholela ya raia, mawakili wa Israel walidai kuwa Hamas ilikuwa ikitumia raia kama ngao za binadamu na kwamba wanajeshi wa Israel walikuwa wakijaribu “kupunguza” madhara kwa raia.
Hata hivyo, kumekuwa na visa vya raia kupigwa risasi na kuuawa huku ni wazi kuwa hawana silaha na wakijaribu kuhama. Katika video ya hivi majuzi, iliyothibitishwa ambayo ilisambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii, bibi wa Kipalestina alionekana akijaribu kupita kwenye njia ya kutoka kaskazini mwa Gaza, iliyotangazwa kuwa salama na vikosi vya Israeli, huku akiwa ameshikana mikono na mjukuu wake wa miaka mitano, ambaye alipeperusha bendera nyeupe. Bibi huyo aliuawa kwa kupigwa risasi ya sniper.
Mwezi Desemba, Israel pia iliwaua raia wake watatu ambao walionekana kutoroka utumwa wa Hamas. Pia walipeperusha bendera nyeupe na kuandika jumbe za SOS zenye mabaki ya chakula. Israel ilijibu hili wakati huo ikisema wanajeshi wake walikuwa wakifanya kazi chini ya shinikizo kubwa na wamefanya makosa.
Mawakili wa Israeli pia walisema Ijumaa kwamba wasiwasi wowote ambao wanajeshi wao “wamekiuka” sheria za vita “utashughulikiwa na mfumo wa kisheria wa Israeli”. Lakini Kumar alisema HRW hapo awali imefichua ushahidi kwamba Israel inaendesha “mfumo wa haki mbovu na usio na usawa”.
“Mamlaka mara kwa mara yameshindwa kuviwajibisha vikosi vyao wakati vikosi vya usalama vinapowaua Wapalestina, wakiwemo watoto, katika mazingira ambayo matumizi ya nguvu ya mauaji hayakuwa halali chini ya kanuni za kimataifa,” Kumar alisema.
Ukosefu wa mamlaka
Shaw alisema Pretoria ilishindwa kuwasiliana na Tel Aviv kuhusu kesi hiyo kabla ya kuwasilisha ombi hilo mahakamani, kama inavyotakiwa na sheria za mahakama yenyewe.
Mwakilishi huyo wa Israel alidai Afrika Kusini ilikuwa imeipa siku chache tu kujibu taarifa kwamba inafanya mauaji ya halaiki. Alisema kuwa Tel Aviv ilikuwa tayari “kuzungumza” lakini wawakilishi wa Afrika Kusini walikuwa wamekataa kwanza ujumbe ulioandikwa kutokana na likizo, na baadaye wakajibu kwamba “hakuna maana” katika majadiliano. Hilo, Shaw alisema, lilizua swali la iwapo kesi hiyo ilipaswa kufika kortini hata kidogo, maana mahakama hiyo inaweza kukosa uwezo wa kutoa uamuzi.
Ili kuwasilisha kesi mbele ya ICJ, ni muhimu kuonyesha kwamba kumekuwa na “mzozo” wa awali kati ya pande hizo mbili, na kwamba zote zinahitaji ICJ kuingilia kati ili kutafsiri ipasavyo Mkataba wa Mauaji ya Kimbari. Afrika Kusini inaweza kulazimika kuthibitisha kwamba iliipa Israel notisi ya awali kwamba inaamini Tel Aviv ilikuwa ikifanya mauaji ya halaiki huko Gaza, na kwamba kulikuwa na “mzozo” au kutokubaliana kati ya pande hizo mbili juu ya mada hiyo, ili kuhalalisha kupeleka kesi hii mahakamani. zote.
Afrika Kusini haijajibu madai kwamba ilikataa mazungumzo kama hayo.
Msaada wa Kibinadamu
Mwakilishi wa Israel alisema madai kwamba inazuia chakula, maji, mafuta na vifaa vingine muhimu kutoka Gaza “si sahihi”, akiongeza kuwa “malori 70” ya msaada wa chakula yaliruhusiwa kuingia Gaza kabla ya vita na idadi hiyo imepanda hadi “106.” lori katika wiki mbili zilizopita”.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, malori 500 ya misaada yalikuwa yakiingia Gaza kila siku kabla ya vita, ambapo Israel ilipiga marufuku misaada yote kuingia. Malori 200 kila siku yaliruhusiwa kuingia wakati wa mapumziko mafupi ya mapigano yaliyokubaliwa kati ya Israel na Hamas, lakini nje ya kipindi cha kusitisha mapigano, malori yasiyozidi 100 yalikuwa yakiingia.
Galit Raguan, kaimu mkurugenzi wa kitengo cha haki ya kimataifa katika Wizara ya Sheria ya Israel, alisema katika mada yake kwamba Hamas inakamata vifaa vya msaada kwa ajili ya wapiganaji wake. Israel, Galit alisema, haikuwa imelenga hospitali, na imesaidia kuwahamisha wagonjwa. Alisema shule, maghala ya Umoja wa Mataifa, na hospitali zimepekuliwa na vikosi vya Israel kwa sababu wapiganaji wa Hamas walikuwa katika maeneo hayo, akiongeza kwamba Israel huwaonya watu kuhusu shambulio linalokuja kupitia simu na kwa kutupa vipeperushi.
Hata hivyo, waandishi wa habari wa Palestina wameripoti mara kwa mara kwamba mashambulizi ya mara kwa mara ya ukanda huo mara nyingi huja bila onyo, na waandishi wa habari wenyewe wakishambuliwa vikali. Hospitali kadhaa zimeshambuliwa kwa mabomu na kuachwa bila uwezo kufanya kazi.
Sammonds kutoka War on Want alidokeza kuwa Israel haikuanza kuzuia ukanda huo Oktoba 7. “Kumekuwa na kizuizi kisicho halali kwa Gaza kwa miaka 16 na tayari ilionekana kama adhabu ya pamoja [kabla ya vita kuanza]. Msaada ambao umekuja [tangu vita kuanza] ni njia ndogo tu ikilinganishwa na kile kinachohitajika,” alisema.
Kumar, katika HRW, aliongeza: “Kwa kweli, vikosi vya Israeli vinazuia kwa makusudi usambazaji wa maji, chakula na mafuta, huku wakizuia kwa makusudi msaada wa kibinadamu, inaonekana wakiharibu maeneo ya kilimo, na kuwanyima raia vitu muhimu kwa maisha yao. Human Rights Watch wamegundua kuwa Israel inatumia njaa kama silaha ya kivita.”
Kifuatacho
Akihitimisha hoja za Israel siku ya Ijumaa, Gilad Noam, naibu mwanasheria mkuu wa Israel wa masuala ya kimataifa, alisema mahakama haipaswi kuamuru hatua za muda (kusimamisha shambulio la Gaza) kwa sababu Hamas inachukuliwa kuwa shirika la kigaidi na Israel na hatua zozote kama hizo zinaweza kusababisha madhara kwa Waisraeli.
ICJ ilisema itatangaza uamuzi wake hivi karibuni, lakini haikutoa tarehe maalum. Kuna uwezekano mahakama itatoa taarifa katika wiki zijazo, wataalam walisema.
Ni ngumu kutabiri mahakama itafanya uamuzi upande gani. Mchambuzi mkuu wa kisiasa wa Al Jazeera, Marwan Bishara, alisema kuwa Israel ilitoa “hoja kali za kimamlaka na kiutaratibu”, akimaanisha madai hayo kutoka Israel kwamba Afrika Kusini haikuipa muda wa kutosha kujibu kabla ya kuwasilisha katika Mahakama ya The Hague. Alielezea sehemu hii ya hoja yake “inaweza kuwa imetia doa” katika kesi ya Afrika Kusini.
Lakini “Israel ilipoteza hoja ya maadili, ukweli, kihistoria na kibinadamu kwa sababu ya jinsi hali ilivyokuwa mbaya Gaza – kwa vifo vya watu na mauaji ya mpangilio huko,” Bishara alisema, akiongeza kwamba juhudi za Israel kuishawishi mahakama kuhusu jinsi inavyoshughulikia hali ya kibinadamu huko hazikufanikiwa.
Mike Becker, profesa wa sheria ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Trinity, Dublin, alisema mahakama itakuwa katika nafasi ngumu: Inaweza isiwe na nia ya kuamuru wanajeshi wa Israel kutoka Gaza wakati haiwezi kutoa amri kama hiyo kwa Hamas, ambayo sio washiriki wa mkataba wa mauaji ya kimbari.
“Afrika Kusini imefanya vya kutosha kukidhi mahitaji,” Becker alisema, akirejelea kesi ya Pretoria kwa amri ya dharura ya kusitisha. “Lakini hatua za muda [mahakama itakazotoa] zinaweza kwa kiasi kikubwa kutaka kushikilia Israeli kwenye ahadi ambayo imefanya leo kuhusiana na misaada ya kibinadamu,” alisema.
Chanzo: Aljazeera