Marekani na Kenya wamesaini makubaliano ya ulinzi yatakayosaidia taifa la Kenya kupata vifaa na msaada wa wanajeshi wakati taifa hilo likijiandaa kuongoza kikosi cha kimataifa cha amani nchini Haiti, ambacho kitasaidia nchi hiyo kuimarisha usalama.
Kwa sasa Haiti inapambana na machafuko yanaoyasababishwa na makundi ya uhalifu na hasa katika mji mkuu wa Port-au-Prince.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na mwenzake wa Kenya, Aden Duale, wamesaini makubaliano hayo katika mkutano uliofanyika jijini Nairobi, Kenya.
Imeelezwa kuwa makubaliano hayo yanajikita katika uhusiano wa kiulinzi kwa miaka mitano ijayo, wakati taifa hilo likiongeza harakati zake dhidi ya kundi la wanamgambo wa Al-Shabaab.
Austin ameishukuru Kenya kwa kujitolea kuongoza ujumbe wa amani nchini Haiti na kusema kwa mara nyingine kwamba Serikali ya Marekani itashirikiana na Bunge ili kupata dola milioni 100 za ufadhili ilizoahidi.
Moja ya makundi yanayotishia usalama nchini Haiti na hasa katika Mji Mkuu wa Port-au-Prince, ni lile linaloongozwa na aliyewahi kuwa ofisa wa polisi Jimmy Charizier maarufu ‘Barbecue, huku yakishinikiza serikali ya Haiti ijiuzulu.