Malawi inakabiliwa na uhaba wa mafuta unaopelekea misururu mirefu ya magari katika vituo vya mafuta yanayosubiri kwa saa kadhaa na wakati mwingine usiku kucha kwa matumaini ya kupata mafuta.
Mtendaji mkuu wa Mamlaka ya udhibiti wa nishati nchini Malawi (MERA) amesema, nchi hiyo imemaliza akiba yake ya mafuta hasa kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni, na wala sio kwamba mafuta yamefichwa na wafanyabiashara ili kupandisha bei.
Uhaba wa mafuta umewalazimu waendesha magari ya umma kupandisha gharama karibu mara mbili ya nauli za zilizozoeleka, lakini bado wanadai licha ya kupanda kwa nauli, hawapati faida yoyote kwa sababu wanatumia siku moja au mbili kupanga foleni ya mafuta bila kufanya biashara yoyote.
“Watu wengi hapa wanategemea mabasi madogo. Kwa hiyo tatizo hili limetuathiri sana kwa sababu hata familia zetu zinaishi kwa sababu ya biashara hii na uhaba wa mafuta ni pigo kubwa kwetu,” amesema mmoja wa wamiliki wa biashara ya mabasi madogo nchini humo.