Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imesitisha ratiba za mabasi 38 ya Kampuni ya mabasi ya New Force yanayoanza safari kuanzia saa 9:00 na saa 11 alfajiri.
Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na hivi karibuni kushuhudiwa ajali za mabasi matano ya abiria ndani ya wiki nne na kusababisha madhara kwa abiria.
Akizungumza Dar es Salaam leo Jumatatu Julai 3, 2023 wakati anatoa uamuzi huo, Mkurugenzi wa Latra, Habibu Saluo amesema kutokana na wimbi la ajali kwa mabasi ya kampuni hiyo, walifanya uchunguzi na kubaini uvunjaji wa sheria kwa makusudi wa kanuni za usafirishaji wa magari.
Kampuni ya New Force ni miongoni mwa watoa huduma waliopewa ratiba za saa 9:00 alfajiri mabasi 10 na saa 11:00 alfajiri mabasi 28 na walipewa sharti la kuhakikisha sheria zinazingatiwa lakini kwa makosa haya tunasitisha ratiba yao,” amesema.
Amesema kuanzia Julai 5 mwaka huu mabasi hayo yatafanya safari zake kuanzia saa 12:00 asubuhi na kuendelea, huku akieleza orodha ya mabasi 38 imeambatanishwa kwenye taarifa waliyopewa na kwamba hatua hiyo siyo adhabu bali ni utaratibu wa kidhibiti ajali unaochukuliwa kwa shabaha ya kuhakikisha usalama wa abiria.