Gazeti la Nation la nchini Kenya limeeleza kuwa maelfu ya wamiliki wa magari pamoja na boda boda katika mji wa mpakani wa Namanga wanaendelea kuingia nchini Tanzania ili kununua mafuta ya bei rahisi.
Kuanzia tarehe Mosi mwezi Julai shirika la kudhibiti bei ya mafuta nchini Kenya EPRA liliongeza bei ya mafuta kwa mujibu wa sheria ya fedha ya mwaka 2023, ambayo iliongeza VAT kutoka asilimia 8 hadi kumi na sita.
Hii ikapelekea Nairobi na kaunti ya Kajiado lita moja ya petroli kuuzwa kwa shilingi 195.5 za Kenya huku nchini Tanzania ikiuzwa kwa shilingi 2,781 za Tanzania ambazo ni sawa na shilingi 160 za Kenya.
Hii ina maana kwamba lita moja ya mafuta ya petroli iko chini kwa shilingi 35 za Kenya nchini kwa nchini Tanzania.
Kulingana na gazeti hilo, bei ya mafuta imekuwa ikishuka nchini Tanzania katika kipindi cha miezi miwili iliopita huku ikipanda nchini Kenya.