Mahakama ya Juu nchini Ghana imeanza mashauriano juu ya pingamizi la sheria dhidi ya LGBTQ+ iliyopitishwa na bunge mapema mwaka huu.
Richard Dela Sky, wakili na mwanahabari, alipewa kibali na mahakama kupinga mswada huo wenye utata, ambao unaweka adhabu kali pamoja na kifungo, kwa watu wanaojitambulisha kuwa LGBTQ+ au kutetea haki za LGBTQ+.
Kesi hiyo iliwasilishwa mwezi Machi kusimamisha maendeleo ya mswada huo, ikiitaka mahakama ya Ghana kuzuia maafisa wa bunge kupeleka mswada huo kwa rais ili kuidhinishwa kuwa sheria.
Pia kesi hiyo ilikuwa na lengo la kumzuia Rais Nana Akufo Addo kupitisha mswada huo sheria.
Siku ya kwanza ya kesi ilikuwa na mvutano na mabishano makali kati ya wawakilishi wa kisheria na Jaji Mkuu wa Ghana Gertrude Torkornoo.
Torkornoo alionyesha kusikitishwa na lugha ya uchochezi inayotumiwa katika baadhi ya maeneo kwenye hati ya kiapo, na kuonya dhidi ya matumizi yake katika mawasilisho yajayo.
Vikao hivyo vilisimamiwa na Jaji Mkuu Torkornoo akiwa na majaji wengine wanne wa Mahakama ya Juu, na kuonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni kutokana na maslahi mapana ya umma.
Rais Akufo Addo ameashiria nia yake ya kusubiri uamuzi wa Mahakama kabla ya kuamua hatima ya mswada huo, ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 17.