Rais wa Marekani Joe Biden ameishutumu sheria mpya ya Uganda inayopinga mapenzi ya jinsia moja na kusema kuwa inakiuka haki za binadamu, na inahatarisha maendeleo ya uchumi wa nchi hiyo iliyoko mashariki mwa bara la Afrika.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa siku ya Jumatatu, Rais Biden alilaani hatua hiyo ya kupitishwa kwa mswaada huo wa sheria wenye utata unaoharamisha mapenzi ya jinsia moja, ikiwa pamoja na adhabu ya hadi miaka 30 jela na faini ya hadi shilingi milioni 10 za Uganda.
Rais Biden alisema “Ninaungana na watu duniani kote wakiwemo watu wengi wa Uganda katika kuitaka sheria hiyo ifutwe mara moja” na kuongeza kuwa, “hakuna mtu anayestahili kuishi kwa kuhofia maisha yake wakati wote au kufanyiwa vitendo vya ukatili na ubaguzi. Ni makosa”
Rais Museveni aliupitisha mswaada huo wenye adhabu kali dhidi ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja kuwa sheria ya ushoga ya mwaka 2023 siku ya Jumatatu, baada ya kufanyiwa marekebisho ambayo vipengele vingi vyenye msimamo mkali havikurekebishwa.