Jiji la Dar es Salaam limeorodheshwa kuwa jiji la 85 kwa utajiri zaidi duniani na la 12 barani Afrika, likichochewa na ukuaji wa idadi ya watu wenye hali ya juu, kwa asilimia 20 katika muongo uliopita.
Ripoti ya Miji Tajiri Zaidi Duniani ya 2023 ya shirika la “New World Wealth and Henley Partners” imeuweka mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania miongoni mwa miji mikuu duniani yenye idadi ya mamilionea inayokua kwa kasi zaidi.
Ripoti hiyo inayofuatilia mienendo ya uhamiaji wa watu binafsi duniani kote, inaonyesha Dar es Salaam ina matajiri 1,400 wenye thamani ya angalau dola milioni 1, na mamilionea 4 (watu wenye utajiri wa zaidi ya dola milioni 100) na mtu mmoja ambaye ni bilionea wa dola.