Kamanda wa Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan ametishia kuunda serikali yake ikiwa jeshi litaanzisha utawala katika mji wa mashariki wa Port Sudan.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Luteni Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, alisema RSF imeonyesha uvumilivu mkubwa kuhusiana na maamuzi ya kibinafsi ya mkuu wa jeshi la Sudan Luteni Jenerali Abdel Fattah al- Burhan.
“Hatutaruhusu mtu yeyote kuzungumza kwa niaba ya Sudan na kudai kuwa ni halali kwake kufanya hivyo,” aliongeza kiongozi huyo wa RSF.
Tishio la kiongozi huyo wa RSF limekuja baada ya ripoti za vyombo vya habari vya serikali kusema kwamba serikali inayoongozwa na jeshi ina mpango wa kujenga ikulu ya Rais na makao makuu ya wizara yake ya mambo ya nje katika bandari ya Sudan kwenye jimbo la Bahari Nyekundu.
Jiji hilo limekuwa likitumika kama kituo cha uendeshaji wa serikali tangu mzozo ulipozuka kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha dharula cha RSF mjini Khartoum katikati ya mwezi Aprili.