Serikali imefafanua kuwa ukarabati wa shilingi bilioni 31 utakaofanyika kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa chini ya kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) ya China utakuwa ni ukarabati wa viwango vya kimataifa.
Akizungumza Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Said Yakubu amesema ukarabati huo utahusisha ukarabati wa vyumba vya wachezaji (dressing room), vyumba vya waandishi wa habari na eneo la watu mashuhuri zaidi (VVIP).
Ameongeza kuwa katika ukarabati huo watabadilisha viti vyote vya uwanja, mfumo wa matangazo wa uwanja (PA system), ubao wa matangazo kuwa wa kidijitali, mfumo mzima wa TEHAMA, marekebisho kwenye eneo la uwanja kwa kuweka magoli mapya pamoja na maboresho kwenye neo la benchi la ufundi.
“Mfumo wa AC katika uwanja mzima utakwenda kurekebishwa, mfumo wa umeme, mfumo wa maji safi na majitaka, tutajenga mkahawa kwa ajili ya mashabiki humu ndani. Kama mnavyofahamu, tunatakiwa tuwe na chumba cha VAR ni katika vitu tunaenda kuweka, na tunaenda kuweka taa mpya,” amesema.
Aidha, katibu mkuu amebainisha kuwa kuna vyumba maalum vinavyolipiwa na watu wasiopenda bughudha (directors box) ambavyo havitumiki ipasavyo, hivyo marekebisho hayo pia yatawalenga watu hao ikiwa ni pamoja na kuwawekea lifti yao mahsusi pamoja na eneo lao la kuegesha magari.