Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mstaafu, Prof. Mussa Assad amesema tatizo lililopo katika suala la ushirikiano wa Tanzania na Dubai kwenye uendeshaji wa bandari ni kuwasikiliza wanasheria ambao hawana utaalamu wa masuala ya uwekezaji.
Amesema hayo wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha habari ambapo amebainisha kuwa suala la uwekezaji wa bandari nchini linatafsiriwa visivyo kutokana na usomaji mbaya wa sheria na kutokuwa na utaalamu na masuala ya uwekezaji.
“Tatizo ni usomaji mbaya, watu si wataalamu wa uwekezaji. Kipengele kinachozungumziwa pale ni land rights (haki za ardhi) haki ya ardhi sio umiliki, ni utumiaji wa ile ardhi, yaani haki ya kutumia na kupata access. Kwa mfano Bandari ya Dar es Salaam mmiliki ni Shirika la Bandari, na ana hati, kwahiyo atampa huyu mtu haki ya kutumia, hawezi kuwa anamiliki, atapata haki ya matumizi tu,” amesema.
Akizungumzia kuhusu suala la ukomo wa mkataba huo amesema hayo ni makubaliano kati ya nchi na nchi, hivyo ukomo utapatikana katika mikataba ya miradi ambayo itakwenda kutekelezwa.