Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa msamaha kwa wafungwa 1,082 na tayari wafungwa 29 wameshaachwa huru.
Taarifa iliyotolewa na Serikali kupitia wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imesema msahama huo wa Rais Samia ni sehemu ya kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.
Aidha kufuatia hatua hiyo ya Rais wafungwa 20 waliohukumiwa adhabu ya kifo, wamebadilishiwa adhabu hiyo na kuwa kifungo cha maisha.
Pia wafungwa wengine 27 waliohukumiwa kifungo cha maisha, wamebadilishiwa adhabu na kuwa kifungo cha miaka 30.
Na wafungwa 1,006 wamepunguziwa adhabu zao, hivyo watabaki gerezani na kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.