Rais wa Misri Abdel Fattah Al-Sisi amewataka wananchi wake kuwa na watoto wachache akisema kwamba kiwango cha sasa cha kuzaliana kitaleta janga kwa nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika.
“Tunahitaji watoto 400,000 wanaozaliwa kwa mwaka,” Al-Sisi aliliambia Kongamano la Kimataifa la Idadi ya Watu, Afya na Maendeleo (Global Congress on Population, Health and Development (PHDC)), ambalo lilifunguliwa mjini Cairo mapema wiki hii.
“Sikubaliani kwamba kuwa na watoto ni suala la uhuru binafsi, Kuacha uhuru huo kwa watu ambao labda hawajui ukubwa wa changamoto, Mwishowe, ni jamii nzima na taifa la Misri ambalo litalipa gharama” Al-Sisi alisema.
Raisi Abdel Fattah alitoa mfano wa China, ambayo ilifanikiwa kudhibiti idadi ya watu kwa kuweka sera kali ya mtoto mmoja katika miaka ya 1970 mpaka ilipofika 2015 na kuanza kuhimiza ongezeko la watu.
Kulingana na mkutano wa PHDC, ukuaji wa idadi ya watu unaweza kuweka mzigo kwenye rasilimali na miundombinu, na kusababisha changamoto za kiafya na kijamii.
Aidha Idadi ya watu inayoongezeka kwa kasi inahatarisha upatikanaji na ubora wa huduma za msingi ikiwa ni pamoja na, afya, elimu, hifadhi ya jamii na kuchangia kupungua kwa kasi kwa maliasili.