Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema kuwa atawania tena muhula wa nne katika uchaguzi wa rais utakaofanyika mwaka ujao.
Kagame ametoa kauli yake hiyo akiliambia jarida la lugha ya kifaransa la Jeune Afrique wakati akifanyiwa mahojiano.
Aidha alipoulizwa kuhusu nchi za Magharibi zitachukulia vipi uamuzi wake wa kugombea tena Rais Kagame alisema,
“Samahani kwa nchi za Magharibi, lakini kile ambacho nchi za Magharibi zinafikuria hilo sio tatizo langu”.
“Nimefurahishwa na imani ambayo Wanyarwanda wanayo kwangu na nitawatumikia daima, kadri niwezavyo.” Aliongeza
Chama tawala nchini humo, Rwandan Patriotic Front (RPF-Inkotanyi), kilimuacha Kagame kuendelea kuhudumu kama mwenyekiti wake ambapo ameongoza chama hicho tangu mwaka 1998.
Kagame amekuwa Rais wa taifa hilo la Afrika Mashariki tangu mwaka wa 2000 na mpaka sasa ana miaka 23 akiwa madarakani.
Rwanda chini ya Rais Kagame imekuwa na utulivu wa kisiasa lakini wakosoaji na makundi ya haki za binadamu yanaituhumu serikali yake kwa kuweka mipaka ya uhuru wa kisiasa na kukandamiza upinzani.