Anaandikia Dkt. Ahmed Sovu
Kwa takribani majuma kadhaa sasa, kumekuwa na mjadala kuhusu mkataba mkuu (makubaliano) wa uwekezaji na uendeshaji wa bandari maarufu kama DP WORLD wenye lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kwenye bandari ya Dar es Salaam.
Kuwapo kwa mjadala wa suala hili kumetokana na msingi mkubwa wa kidemokrasia ulowekwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa aghalabu akipenda kutumia falsafa yake 4R na kuwataka viongozi wanaomsaidia kutumia falsafa hiyo katika kufikia uamuzi wa aina mbalimbali.
Tumeona makala nyingi sana, vipane vya video, Waheshimiwa Wabunge, wataalamu na wachambuzi mbalimbali nao wameandika na kulijadili jambo hili kwa namna mbalimbali.
Wapo wanasheria, wachumi, wanasiasa na wengineo wote walifafanua kwa njia anuwai.
Katika uchambuzi wetu tumejikita katika mjadala huu wa bandari kwa kuzingatia misingi ya falsafa ya 4R.
Falsafa ya 4R ni ipi?
Falsafa ya 4R, iliasisiwa na Dkt.Samia Suluhu na inayo misingi mikuu minne, nayo ni Reconciliation (maridhiano), Resilience (ustahamilivu), Reform (mabadiliko) na Rebuilding (kujenga upya).
Baada ya sisi kupitia mkataba huu, kusikiliza maoni ya wabunge, viongozi wa vyama vya siasa, wanataaluma, wanahabari na wadau mbalimbali.
Hivyo, tunaonesha kusadifu kwa nadharia hii katika kuliendea jambo hili.
Hapa chini tunafafanua misingi ya nadharia hii na ni kwa namna gani kila mmoja ulivyoweza kutumiwa katika kuchangia maboresho na kuelewa makubaliano au mkataba huo.
Reconciliation(Maridhiano)
Maridhiano ni hali ya kukubaliana kwa watu, makundi au mataifa zaidi yaliyokuwa katika mgogoro.
Mgogoro haina mana ya fujo tu pekee. Mgogoro ni hali ya mkwamo wa jambo.
Ni dhahiri shahiri kuwa katika shughuli za utendaji wa bandari yetu ya Dar es Salaam kumekuwa na mkwamo wa utendaji na ufanisi wa kuridhisha.
Katika hali kama hiyo, historia inaonesha Viongozi wetu wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto hizo. Hatua hizo zimekuwa zikizaa matunda lakini kwa kiwango kisichoridhisha na bado kumeendelea kuwa na mkwamo.
Kutokana na hali hiyo, serikali yetu ilichukua hatua muhimu za kutafuta dawa ya kudumu kwa kutafuta mwekezaji mahiri ambaye atatatua changamoto hizo.
Kwa hivyo, kupitia majukwaa ya kimataifa ilipata mshirika aliyeonesha raghba (interest) kufanya uwekezaji na uendeshaji wa pamoja ili kuongeza ufanisi.
Kufikia hatua hii, kuna hatua mbalimbali za kuje maridhiano zilichukuliwa ikiwa ni pamoja na kuunda timu ya wataalamu iliyosimamia mchakato mkataba wa unaojenga maridhiano na mashirikiano baina ya nchi hizo mbili.
kwa baadaye hatua nyingine kwa ngazi tofauti tofauti kama vile kwa waheshimiwa wabunge, baraza la mawaziri, maoni ya wananchi (public hearing) ziliendelea.
Hatua zote hizi zililenga kupata maridhiano na uwelewa wa pamoja kadri ya sheria zetu.
Huu ndio msingi wa kwanza wa falsafa ya R4 ulivyojengwa katika suala hili.
Ni muhimu sana kujenga maridhiano, maelewano ya pamoja kama nadharia hii inavyosisitiza.
Resilience/ Ustahamilivu
Msingi wa 2 wa falsafa ya R4 ni Ustahamilivu.
Ustahamilivu ni hali ya kuweza kuvumilia jambo.
Msingi huu ni msingi mzito sana ambao unaendana na mambo mengi sana.
Miongoni mwayo ni uvumilivu, subira, utu, uzalendo, utaifa na kutanguliza maslahi ya taifa mbele.
Katika mjadala wa uwekezaji wa Bandari, wapo wazalendo ambao wameweza kutoa maoni yao kwa nia thabiti ya kujenga na kupata mikataba bora zaidi ambayo itakuwa na masilahi mapana ya nchi.
Wapo waliyoyapitia kwa utondoti makubaliano haya kati ya serikali ya Tanzania na Dubai na wakawasilisha kwa njia bora zenye kujenga na zenye msingi wa ustahamilivu.
Mathalan, Chama cha wanasheria Tanzania, TLS binafsi niliona waraka wao ambao kwa hakika ulijikita katika kuujadili mkataba wenyewe na si mambo mengine.
Lakini msingi huu wa ustahamilivu kwa baadhi ya watu mambo yalikuwa kinyume sana.
Kila Mtanzania aliyefuatilia mjadala huu amesikia.
Maana mjadala ulihamishwa kutoka katika taaluma za kisheria, uwekezaji na uchumi na kwenda katika mambo yanayoturejesha nyuma ya kibaguzi.
Waliokuwa wanayafanya haya ni watu watajika katika jamii yetu, wana uluwa wao, wana nafasi zao lakini kwa masikitiko makubwa wanaubadili mjadala pengine kwa malengo yao.
Tumesikia na kuona wakianza kuleta masuala ambayo yanawabagua Watanzania kwa maeneo yao, kwa dini zao, kwa makabila yao na kwa rangi zao.
Jambo hili ni hatari sana. Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere amewahi kulikemea hili na kulipiga vita sana suala ubaguzi wa ainya yoyote ile.
Tumeshuhudia lugha zisizo za staha, zisizoleta Mshikamano na za kibaguzi kwa watu binafsi badala ya kujielekeza kwenye hoja. Hili ni jambo baya sana kwa Taifa.
Unajiuliza ni kweli mkataba tu wa bandari au kuna yaliyojificha nyuma ya pazia?? Maana haiyumkiniki kuona watu wenye uluwa na satua kuyafanya haya.
Ni faraja tu kuwa baadhi ya viongozi na wananchi wameyaona haya na kuanza kuyakemea.
Katika falsafa hii ya 4R huu msingi wa ustahamilivu ni muhimu sana.
Bila ustahamilivu, uvumilivu, subra hakuna mwafaka katika jambo jema la aina yoyote ile bila ya kuwa na uvumilivu.
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu wakati anatoa idhini na kuondoa zuio la kurejesha mikutano ya hadhara alisema tunamnukuu;
Tunatoa ruhusa ya vyama vya siasa twendeni tukafanye siasa, tukafanyeni siasa za kupevuka, tukafanyeni siasa za kujenga na si kubomoa..
Dkt. Samia ni kama alitabiri na kusisitiza kuwa sio kuwa hataki kukosolewa la hasha, kwani chama chake cha CCM kina utamaduni wa kujikosoa.
Hivyo, aliwataka wanaotaka Kukosoa wajizatiti na kuonesha zaidi changamoto ili yeye na viongozi wenzake wazitafutie majawabu kadri iwezekanavyo.
Vinginevyo wasitukane na kutoa kashfa kwani yeye anaweza kuvumilia ila mashabiki wake au chawa wake hawatakubali.
Alitanabaisha kwa kusema:
Samia Suluhu anaweza kuwa na upeo mkubwa wa ustahamilivu, mshabiki wake, chawa wake anaweza asistahamili akaja akavaana na chawa wako wewe aliyetukana, balaa likaanzia hapo
Hata mwaka haujaisha haya yamedhihirika hasa katika sakata la mjadala wa bandari. 😎😎
Tunawanasihi Watanzania wenzetu kuendelea kuushika ipasavyo mhimili huu wa ustahamilivu kwa kujenga hoja na sio kuleta viroja.
Tuna hakika tutazidi kujenga jamii bora na kusaidia viongozi wetu kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Hata hili la bandari kupitia mikataba mahsusi itakayoingiwa, bila shaka maoni na mapendekezo bora ya kujenga yataingizwa humo.
Reforms/Mageuzi
Mageuzi ni mabadiliko ya hali fulani katika jamii.
Falsafa ya 4R kupitia msingi huu wa mageuzi inasisitiza mabadiliko.
Baada ya maridhiano, ustahamilivu hatua inayofuata ni ya Mageuzi.
Katika suala hili la uwekezaji wa Bandari ni dhahiri kwamba kila Mtanzania amekuwa akisikia na kujua udhaifu ulikuwapo bandarini. Katika awamu mbalimbali za uongozi kama tulivyoeleza hapo juu.
tumeona, kupitia ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, na taarifa mbalimbali juu ya hali hiyo.
Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia falsafa hii ya 4R anasisitiza suala la mageuzi ili kufikia ufanisi utakiwao.
Juhudi za serikali yake ni kulenga kufanya mageuzi makubwa ya kiutendaji katika bandari na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Uamuzi huo unao msingi katika sera zetu na ilani.
Kwa kawaida mageuzi sio jambo jepesi. Mageuzi ni jambo gumu na wakati mwingine hutia hofu.
Ndio maana baadhi ya Watanzania wazalendo wa kweli wenye mapenzi ya kweli ya nchi wakapata hofu na kutaka kujua kwa kina juu ya uwekezaji huu wa bandari.
Ila wapo waliopatwa hofu tunadhani si kwa sababu za Kizalendo, pengine ni kwa sababu kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakinufaika na mianya iliyopo hapo bandarini.
Hapa tumeshuhudia hoja mbalimbali zikiibuka katika mijadala na wataalamu wa serikali waliohusika katika kadhia hii wakijibu hoja hizo.
Kwa upande wetu katika makala haya tunadondoa baadhi ya hoja ambazo ziliwatia hofu Watanzania lakini wataalamu wa serikali, wanasheria nguli na msemaji wa serikali wameweza kuzijibu na kudadavua kwa utuo na utuvu.
(i) Ukomo wa mkataba
Katika siku za mwanzo kabisa za mjadala huu tulisikia kuwa mkataba huu utakuwa wa miaka 100.
Baadaye wanasheria akiwamo Mwanasiasa na mwanasheria Tundu Lisu wakafafanua kuwa katika makubaliano hayo hakuna kifungu kinachoonesha mkataba huu kuwa ni wa miaka 100
Baada ya hapo tukaskia tena ni wa milele🤣🤣 dah!
Wataalamu wakasema hapana mkataba huu mkuu na mingine itakayoingiwa sio ya milele bali itakuwa ikifanyiwa mapitio (review) na tathmini kwa kuzingatia ufanisi wa mwekezaji (KPI) Yaani, Key Performance Indicators ambazo zitaamua aendelee au la.
Pia, wameeleza kuwa katika ile mikataba mahsusi kutakuwa na ukomo kutegemeana na eneo linalohusika.
(ii) Ajira za wafanyakazi Watanzania
Wataalamu hao wameeleza kinagaubaga kuwa hakuna Mtumishi wala mfanyakazi wa bandari atakayepoteza ajira yake.
(iii) Mwekezaji atachukua bandari zote
Hoja hii ilijibiwa na
Wataalamu hao, kuwa sio kuwa watachukua bandari zote la hasha ni ya Dar.
Hata hiyo ya Dar es Salaam ni kwa sehemu kadhaa tu.
(iv) Dubai si nchi
Hii ni hoja nyingine iliyotajwa. Wataalamu hao wamefafanua kuwa huu mkataba wa IGA, yaani Inter government Agreement ni baina ya nchi mbili zenye mamlaka kamili.
Wameeleza kuwa Dubai ni nchi miongoni mwa nchi 7 zinazounda Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E).
Hivyo, hapana shaka juu ya hilo na makubaliano yaliyoingiwa kinchi ni sahihi.
(v) Kwa nini wasiwekeze Watanzania
Hili nalo limelezwa kuwa uwekezaji huu si uwekezaji tu. Uwekezaji huu ulihitaji mwekezaji mahiri.
Mbali ya mwekezaji kuwa fedha pia suala la tajriba na uzoefu wa kazi ni muhimu sana.
Wataalamu hao wamumueelezea DP WORLD 🌎 kama kampuni kongwe na yenye tajriba pana kwani inaendesha bandari zaidi ya 80 duniani.
(vi) Kwa nini itumike sheria ya Uingereza katika kusimamia mkataba huu
Wanasheria hao wabobezi wamedadavua kuwa mkataba wa nchi mbili hauwezi kufungwa na sheria ya nchi mojawapo zilizopo katika makubaliano hayo.
Hivyo, Sheria za Uingereza ambazo pia kwa kiasi kikubwa tumezirithi zitatumika. N.k
Kwa hivyo, hapa tunabaini kuwa msingi wa kwenda kwenye mageuzi si mwepesi ni lazima kufanyike mijadala ya kina ili kujenga maridhiano na uvumilivu ili kufikia mageuzi ya kweli.
Rebuilding/Kujenga upya
Huu ni msingi wa 4 katika falsafa hii ya 4R. Msingi huu ni muhimu sana.
Baada ya maridhiano, uvumilivu, ustahamilivu na kuangalia namna bora ya kufanya mageuzi ndipo sasa tunaingia kwenye kujenga upya.
Changamoto za kupoteza mapato bandarini, mianya ya rushwa na ufanisi wa wastani, makasha kuchelewa kupakuliwa, kodi kubwa n.k lazima kuangalia ni kwa namna gani tunajenga upya na kufikia ufanisi utakiwao.
Kwa hivyo, kwa kuzingatia msingi huu wa kujenga upya serikali imetuhakikishia kuwa kupitia uwekezaji huu kutakuwa faida nyingi ambazo zinakwenda kuifanya bandari ya Dar es Salaam kuwa mpya na yenye faida lukuki.
Baadhi ya faida za uwekezaji huo ni hizi zifuatazo;
- Ongezeko la shehena kwa asilimia 158
- Kupunguza muda wa kuondosha mizigo kutoka saa 12 hadi saa 1.
- Kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 5 hivi sasa hadi saa 24 tu.
- Uwekaji wa mifumo ya kisasa ya TEHAMA
- Ongezeko la mapato ya serikali kupitia kodi ya forodha-kutoka Trilioni 7.76 hadi 26.7 ifikapo mwaka 2032/2033.
- Kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo kutoka nchi za nje kwenda nchi jirani. Kutoka dola 💰12,000 hadi 6,000.
- Kuchochea ukuaji wa sekta ya miundombinu
- Kuchochea ukuaji wa sekta ya kiuchumi
- Kupata fursa za mafunzo na kuongeza ujuzi
- Kupata teknolojia ya kisasa zaidi ya kuhudumia meli
- Kuwa na ongezeko la idadi ya meli kutoka meli 1,569 hadi 2,950 ifikapo 2033.
- Kupungua muda wa kushusha makasha kutoka siku nne na nusu hadi siku mbili.
- Kuongezeka kwa ajira kutoka 28,990 hadi 71,990 ifikapo 2032/2033.Unafuu wa bei za bidhaa kwa mlaji wa mwisho. Kwa kuwa mizigo itatoka kwa wakati na kwa muda uliopangwa ni dhahiri itakuwa rahisi kwa wafanyabiashara kuweka bei nzuri kuliko mzigo unapokaa sana kwani humuongezea gharama hivyo hulazimika kupandisha bei ili afidie jambo ambalo humuongezea mzigo mwananchi wa kawaida. N.k
Kwa hakika huku ndio kujenga upya kwa bandari yetu.
Kwa hakika hii ni mfano uliodhahiri unaonesha falsafa ya 4R ya Dkt.Samia ambapo dhamira yake ni kuendeleza mshikamano, upendo, kuvumiliana katika kujenga Taifa la Tanzania yenye sauti moja kuu duniani.
Ni lazima tukubali, tustahamiliane na kuishi huku tukiijenga upya Tanzania yetu.
Ni dhahiri kuwa mijadala yetu itakuwa na hoja za kiushawishi na iliyosheheni hoja zenye kulenga kusaidia wananchi badala ya zile za kuzodowana.
Maoni yetu ya jumla
- Kwanza ni kuomba serikali kuendelea kutoa elimu kwa umma ila Watanzania ambao bado wana hofu au hawajaelewa vema mkataba mkuu na mikataba mahsusi itakayoingiwa waendelee kupewa elimu.
- Tumefurahishwa sana na mkutano ulioandaliwa na wizara ya uchukuzi kwa kukutana na viongozi wa dini, jana pia kukutana na wanahabari.
- Hii mikutano iendelee na hata ikiwezekana kuwe na makongamano ya wazi ili elimu ya jambo hili ipatikane na kuachana na wapotoshaji ambao tunadhani wana malengo yao binafsi.
- Kwa kuwa mkataba mkuu (agreement) umekwishasainiwa na Bunge letu tukufu limeridhia basi na Kazi Iendelee.
- Walioko kwenye timu hatuna shaka wataendelea kuwa imara na kusimamia maslahi mapana ya taifa.
- Maoni yaendelee kupokelewa kama alivyosema mtaalamu wa serikali maoni mengi takriban asilimia 90 yanahusiana na mikataba mahsusi (contracts) itakayoingiwa na si mkataba mkuu (makubaliano) haya yalikuwa yakijadiliwa.
- Tunawanasihi viongozi wetu na wananchi wanaotoa maoni yao waendelee kutumia lugha za staha, za Mshikamano na zenye kujenga zaidi kuliko kubomoa. Amani yetu, umoja wetu na mshikamano wetu ni wa muhimu sana kuliko kitu chochote.
Tunaendelea kumpa maua yake Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kwa falsafa yake ya 4R ambayo inasisitiza kujenga siasa za Kistaarabu zenye kuheshimu haki, Uhuru, Umoja, Usawa na Mshikamano wa watu
Dunia ya leo ni ya siasa ya Kileberali inayojengwa na jamii yenye uvumilivu na ustahamilivu.
Hata hivyo, kwa kipindi cha muda wa miaka 2 tu. Tumeona Dkt.Samia alivyofanya mambo makubwa katika sekta ya utalii kupitia filamu ya The Royal Tour, idadi ya watalii imeongezeka sana, katika sekta ya elimu kujenga madarasa lufufu, kapandisha Boom kwa wanafunzi wa vyuo, mradi wa HEET unaojenga vyuo vikuu katika mikoa isiyokuwa na vyuo.
Kaongeza mishahara na kupandisha vyeo kwa wafanyakazi, kaendeleza miradi yote mikubwa ya kimkakati, sekta ya kilimo, miundombinu barabara kila kona, sekta ya michezo, sanaa na utamaduni, kaongeza ndege ya abiria na mizigo, kanunua mabehewa mapya, karuhusu uhuru wa maoni, anajenga meli, kasambaza umeme kila pahala, kakuza Diplomasia na uchumi, ameunda tume ya haki jinai ili kutetea haki za watu n.k halafu leo aibuke mtu kisa maoni aanze maneno maneno kwa Rais haa! hii hapana.
Tumeshuhudia jana alipovunja ukimya juu ya mjadala huu.
Ametumia lugha za staha na zenye kuamsha Watanzania juu ya vita ya kiuchumi iliyoko mbele yetu.
Kwamba wakati sisi tunalumbana na maneno wenzetu wanachukua hatua na kusonga mbele.
Aidha, amesisitiza wenye maoni thabiti wangaliwe ili tupate timu imara zaidi itakayokamilisha malengo.
Kama alivyonena;
Tanzania ni yetu wote, wote tufikiri, tukawaze kwa ajili ya nchi yetu
Huyu ndio Dkt. Samia Mwanademokrasia.
Mwisho tunaendelea kuwaomba Watanzania, kuendelea kumuamini Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kumuunga mkono kwani ana dhamira njema sana kwa Watanzania na ana nia thabiti wa kuwatumikia Watanzania katika nyanja mbalimbali za maisha.
Mola azidi kumpa siha na ujasiri wa kufanya zaidi ya haya.
Mwandishi ni Mhadhiri na Mshititi kutoka
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
Kampasi Kivukoni.