Watu 10 wamepoteza maisha leo Jumamosi Aprili 8, 2023 katika Kaunti ya Migori nchini Kenya kutokana na ajali ya lori ambalo inaelezwa lilifeli breki na kuparamia kijiwe cha bodaboda.
Watu hao waliopoteza maisha inaelezwa ni vijana wa bodaboda waliokuwa wakisubiria wateja kwenye kijiwe chao.
Taarifa ya awali kupitia mtandao wa Tuko nchini Kenya imeeleza kuwa lori hilo la kubeba mchanga, lilipoteza mwelekeo na kugonga kundi la bodaboda ambao walikuwa pembezoni mwa barabara wakisubiri abiria.
Mashuhuda wa ajali hiyo wamesema muda mfupi eneo hilo lilitapakaa damu na miili ya watu ambapo juhudi za kuwaokoa waliopata majeraja zilikuwa zinaendelea.