Benki Kuu ya ya Tanzania (BOT) inatarajia kuwawezesha mitaji wachimba madini nchini ili kuongeza uzalishaji wa dhahabu ambayo itanunuliwa na Benki hiyo.
Hayo yamesemwa wilayani Bukombe, Mkoani Geita na Waziri wa Madini Anthony Mavunde akihutubia mkutano wa wananchi wa waliojitokeza kumpokea Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Dotto Biteko.
Mavunde amesema serikali inaandaa mpango kupitia mfuko wa dhamana (Export Credit Guarantee Scheme) ili kuangalia namna ambavyo itawasaidia wachimbaji wadogo kupata fedha.
“Lengo wapate fedha, wachimbe na kuuza kwenye viwanda vya kusafisha dhahabu ili itakapo chujwa iweze kuuzwa kwa Benki Kuu.” Amesema Mavunde.
Aidha, ametoa siku tano kwa wataalamu wa serikali kuhakikisha wanakamilisha mpango huo ili kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuitaka BOT kununua dhahabu kwa wachimbaji wa Tanzania kwa utaratibu mzuri.
Kwa upande wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Dotto Biteko ameitaka Wizara ya Madini na BOT kuharakisha zoezi la ununuzi wa dhahabu wa kilo 6000.