Agnes James (36) amefariki dunia huku watu wengine saba wakinusurika kifo kufuatia ajali ya moto iliyotokea katika nyumba waliyokuwa wakiishi.
Tukio hilo limetokea katika Mtaa wa Mwasele “B”, uliopo Kata ya Kambarage, ndani ya Manispaa ya Shinyanga.
Moto huo ulizuka ghafla na kusababisha taharuki kubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, ambao walijaribu kwa juhudi zao za awali kuuzima kabla ya msaada wa kitaalamu kufika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga, chanzo cha ajali hiyo ni shoti ya umeme.
Shoti hiyo ilitokana na matumizi ya vyombo vingi vya umeme kwa wakati mmoja katika soketi za umeme, hali iliyopelekea mfumo wa umeme kushindwa kuhimili mzigo huo na kusababisha moto kuwaka.
Jeshi la Zimamoto limeeleza kuwa, licha ya juhudi za pamoja kati ya wakazi na askari wa zimamoto, haikuwezekana kuokoa maisha ya mama huyo.
Sababu kuu ni ukubwa wa moto uliokuwa unateketeza mali mbalimbali ndani ya nyumba kwa kasi kubwa, hali iliyozuia operesheni ya uokoaji kufanyika kwa mafanikio.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limewataka wananchi kuzingatia matumizi salama ya vyombo vya umeme majumbani, pamoja na kuchukua tahadhari zote muhimu ili kuepuka majanga yanayoweza kuzuilika.



