Raisi wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewasilisha muswada unaopendekeza kuanzishwa kwa vikwazo vikubwa dhidi ya Iran kwa miaka 50.
Muswada huo unapendekeza kupiga marufuku kabisa shughuli za biashara zinazohusiana na jeshi la Wairan, na pia vizuizi vya biashara za huduma kama vile usambazaji, uuzaji, uhamishaji, uzalishaji na matumizi ya bidhaa.
Mapendekezo mengine ni pamoja na kupiga marufuku uhamishaji wa teknolojia na haki miliki kwa wakazi wa Iran, marufuku ya uwekezaji nchini Iran na kwa ajili ya wakazi wa nchi hiyo, na kusitishwa kwa huduma za malipo ya kielektroniki zinazotolewa kwa wakazi wa Iran.
Baraza la Mawaziri, Huduma ya Ujasusi wa Kigeni, Huduma ya Usalama, Benki ya Kitaifa ya Ukraine na vyombo vingine vya serikali vinatakiwa kuteuliwa kuwajibika kwa utekelezaji na ufuatiliaji wa vikwazo hivyo, kulingana na mapendekezo hayo.
Sababu ya vikwazo hivyo ni Ukraine na nchi za Magharibi zina imani kuwa Iran inaipatia Urusi zana za kijeshi, zikiwemo ndege zisizo na rubani ambazo hutumika kuishambulia miundombinu ya kiraia na kijeshi ya Ukraine hata hivyo Iran na Urusi zinakanusha hili.