Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico amefikishwa hospitali akiwa mahututi, baada ya kufeli kwa jaribio la kumuua siku ya jumatano katika mji wa Handlova.
Inaoyesha jaribio hilo la kutaka kumuua kiongozi huyo lina msukumo wa kisiasa kutokana na taarifa ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo.
Fico mwenye miaka 59 alipigwa risasi tano, hali iliyofanya kuwa mahututi na kufanyiwa upasuaji wa saa kadhaa.
Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya Fico kumaliza kikao cha serikali alipotoka nje jengo la mkutano.
Baada ya shambulio hilo aliwahishwa hospitali ya karibu na baadae kusafirishwa kwa helikopta hadi Mji Mkuu wa kikanda wa Banska Bystrica.
Kutokana na hali mbaya ya kiafya walihofia kumsafirisha hadi Bratislava, Mji Mkuu wa Slovakia, kwa kuwa iliwalazimu kumfanyia upasuaji haraka.
“Jaribio hili la mauaji lilikuwa na motisha za kisiasa na uamuzi wa mhalifu ulitokana moja kwa moja baada ya uchaguzi wa urais,” alisema Sutaj Estok, akirejelea uchaguzi wa Aprili ambao mshirika wa Fico alishinda.
Shahidi wa tukio hilo alieleza vyombo vya habari kuwa alisikia milio mitatu au mine ya risasi wakati Fico akitoka kwenye jengo kuwasalimu watu waliokuwa wakimsubiri. Kisha polisi walimkamata mwanaume mmoja na kumzuia akiwa chini.