Mkutano wa maafisa wa ngazi za juu unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo nchini Botswana, utawakusanya wakuu wa majeshi kutoka mataifa karibu 30 barani Afrika.
Mkutano huo wa siku mbili umeandaliwa na Kamandi ya Jeshi la Marekani Barani Afrika (AFRICOM), na ni wa kwanza kufanyika Afrika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017.
“Lengo kuu ni kushughulikia masuala muhimu ya kiusalama yanayokabili bara hili na kwa pamoja kupanga njia kuelekea Afrika salama zaidi” alisema msemaji wa AFRICOM, Luteni Kamanda Bobby Dixon.
Ajenda za mkutano huo itajumuisha mada mbalimbali zikiwemo juhudi za kukabiliana na ugaidi, vitisho vya usalama wa mtandao na misheni za ulinzi wa amani.
Viongozi wa kijeshi na wataalam wa sekta hiyo watajadiliana na kubadilishana maarifa, mikakati, na kuunda ushirikiano wenye lengo la kuimarisha uwezo wa pamoja juu ya ulinzi wa Afrika.
AFRICOM inaona kuwa mkutano huu ni hatua kubwa na muhimu katika kupanga na kutekeleza mbinu za pamoja katika kulinda bara la Afrika.
Kumekuwa na mikutano mingi inayowahusisha wakuu wa majeshi barani Afrika, na wa mwaka jana uliofanyika jijini Roma nchini Italia umeweka kurekodi ya mahudhurio baada ya kuhudhuriwa na nchi 43.