Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limewataarifu wafanyakazi nchini kuwa Serikali imeahidi kukamilisha suala la nyongeza ya mishahara ya kila mwaka kupitia mishahara itakayotolewa kwa wafanyakazi mwezi Agosti mwaka huu.
TUCTA imesema tarifa hiyo ni baada ya kikao cha pamoja ilichokaa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kupatiwa ufafanuzi wa jambo hilo.
Imeongeza kuwa Serikali ilitarajia kutekeleza ahadi hiyo iliyoahidiwa na Rais Samia Suluhu katika sherehe za Meil Mosi mwaka huu katika kipindi cha mwezi Julai, lakini kutokana na sababu mbalimbali zilisababisha kuchelewa kwa utekelezaji huo.
“TUCTA kikiwa chombo chenu kinachowawakilisha wafanyakazi kwenye majadiliano na Serikali kitaendelea kufuatilia utekelezaji wa jambo hili na kuwapa taarifa sahihi kadri zinavyopatikana,” imesema TUCTA.
Aidha, shirikisho hilo limemshukuru Rais Samia na timu yake kwa kutekeleza kikamilifu baadhi ya ahadi alizotoa kwa wafanyakazi katika kipindi cha takribani miezi mitatu.