Chama cha upinzani cha Azimio La Umoja One nchini Kenya kimesimamisha maandamano yake dhidi ya serikali yaliyokuwa yamepangwa kufanyika nchi nzima siku ya Jumatano wiki hii.
Kupitia taarifa iliyotolewa na chama hicho imesema badala ya kwenda mitaani, watashiriki maandamano ya mshikamano na maombi kwa ajili ya waathirika wa ukatili wa polisi katika maeneo mbalimbali nchini.
Chama kimewaomba wafuasi wake kujitokeza kwa wingi na kuwasha mishumaa na kutandaza maua kwa ajili ya watu waliopoteza maisha yao wakati wa maandamano.
Chama hicho kinachoongozwa na Raila Odinga, kimesema hadi sasa vifo 50 vimeripotiwa na wengine kadhaa wamejeruhiwa na wamelazwa hospitalini kutokana na majeraha mabaya.
“Tumeamua kwamba Jumatano badala ya kwenda mitaani kwa maandamano ya amani kama ilivyotangazwa awali, tutafanya maandamano ya mshikamano na maombi kwa ajili ya waathirika wa ukatili wa polisi katika maeneo mbalimbali nchini,” taarifa hiyo imeeleza.