Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza imesema itapiga marufuku uagizaji wa almasi za Urusi kama sehemu ya vikwazo vyake vya hivi karibuni vya kupinga uvamizi uliofanywa na Urusi nchini Ukraine.
Uagizaji wa shaba, aluminium, na nikeli zenye asili ya Kirusi pia utapigwa marufuku chini ya sheria itakayopitishwa mwaka huu.
Kulingana na serikali ya Uingereza, mnamo 2021 kiasi cha mauzo ya tasnia ya almasi ya Urusi ilifikia dola bilioni 4.
Pamoja na hatua hizi, serikali ya Uingereza pia inatayarisha vikwazo vipya dhidi ya watu binafsi na makampuni 86 ya ziada katika eneo la kijeshi na viwanda vya Urusi, pamoja na yale yanayohusishwa na vyanzo muhimu vya mapato kama vile nishati, madini na usafirishaji.
“G7 inasalia kuwa na umoja katika kukabiliana na tishio kutoka kwa Urusi na kuunga mkono Ukraine bila kuyumba,” alisema Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak, ambaye yuko Japan kwenye mkutano wa G7.