ZINAZOVUMA:

Ugonjwa wa Marburg, historia, dalili na tiba yake.

Ifahamu Marburg, asili yake, ilipotokea lakini pia athari na namna...

Share na:

Imeandikwa na Issa Rubajuma “Kabagambe”

Hivi karibuni nchi ya Tanzania imekumbwa na ugonjwa wa ajabu uliyoibuka mkoani Kagera. Ugonjwa ambao umeilazimu serikali kupitia Wizara ya Afya kutoa tahadhari juu ya uwepo wake ambao ulihusishwa na vifo vya watu saba mkoani humo. Huu ni ugonjwa mpya na ni mara ya kwanza kulikumba Taifa, ujulikanao kwa jina la Marburg. Ni ugonjwa Unaotajwa kutokuwa na tiba mahususi bali hutibiwa kwa dalili anazokuwa nazo mgonjwa. Kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Mh. Ummy Mwalimu (MB) uchunguzi wa Maabara ya Taifa umethibitisha uwepo wa virusi vya Marburg ambavyo vinasababisha ugonjwa wa Marburg Virus Disease (MVD) katika Mkoa wa Kagera. Mbali na kugundulika nchini Tanzania, pia kuna baadhi ya nchi za Afrika zilishawahi kufikwa na ugonjwa huo kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Afrika Kusini, Uganda, Zimbabwe.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, virusi vya Marburg, ambavyo hufananishwa na virusi hatari vya Ebola, viligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1967 huko Marburg na Frankfurt, Ujerumani na Belgrade huko Serbia baada ya watu 31 kuambukizwa, ambapo saba kati yao walifariki. Virusi vya Marburg vilipatikana kwa mara ya kwanza kwa tumbili wa kijani kibichi wa Kiafrika walioagizwa kutoka Uganda. Lakini virusi hivyo vimehusishwa na wanyama wengine tangu wakati huo. Kwa binadamu, ugonjwa huo huenezwa zaidi na watu ambao wamekaa kwa muda mrefu katika mapango na migodi iliyo na popo.

Jinsi unavyoambukiza ?

Ugonjwa huu huambukizwa kutoka kwa Binadamu mmoja kwa mwingine hususani kwa njia ya kugusa majimaji ambayo yanaweza kuwa mate , mkojo, damu, machozi au kinyesi yatokayo kwenye maiti au Mgonjwa mwenye dalili, maambukizi pia yanaweza kutoka kwa Wanyama kwenda kwa Binadamu iwapo Mtu atakula au kugusa mizoga au Wanyama walioambukizwa.

Dalili zake ni zipi ?

Dalili za ugojwa wa Marburg huanza ghafla, homa, kuumwa vibaya na kichwa, kuumwa na misuli, baada ya siku tatu kuna dalili nyingine huanza kujitokeza, kuharisha, kuumwa na tumbo,kichefuchefu, kutapika. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwonekano wa wagonjwa katika awamu hii umeelezewa kuwa unaonyesha sifa za ‘kama mzimu’, macho ya ndani, nyuso zisizo na hisia na uchovu mwingi. Baadhi ya watu hutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili na kufa siku nane hadi tisa baada ya kuugua kwa sababu ya kupoteza damu nyingi na mshtuko. Kwa wastani, virusi huua nusu ya walioambukizwa, WHO inasema, lakini aina hatari zaidi imeua hadi 88% ya wagonjwa.

Je ugojwa huo unatibika?

Mpaka sasa hakuna chanjo iliyoidhinishwa ya ugonjwa wa Marburg, japo kuna chanjo mbalimbali ambazo zinaendelea kutengenezwa na WHO kwa kushirikiana na wadau wengine ambao wanaangalia fursa ya kuweza kuzipata iwapo kutakuwa na mlipuko wa ugonjwa huo. Madaktari wanaweza kupunguza dalili kwa kuwapa wagonjwa waliofika hospitali maji mengi ili kuchukua nafasi ya damu iliyopotea, na mara nyingi hutibu chanzo cha ugojwa huo.

Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa Marburg kwa mujibu wa wizara ya afya ;
– Epuka kugusa majimaji ya mwili wa mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Marburg mfano, damu, mate, matapishi, jasho, mkojo au na kinyesi,
– Epuka kugusa au kuosha maiti ya mtu aliyefariki kutokana na ugonjwa wa Marburg bila kutumia vifaa kinga,
– Epuka kugusana na mtu mwingine mfano kusalimiana kwa kupeana mikono, kukumbatiana au kubusiana.
– Nawa mikono kwa maji tiririka na sabuni
– Epuka kula au kugusa mizoga au Wanyama mfano, popo, nyani, tumbili au swala wa msituni.
– Wahi au muwahishe mtu mwenye dalili za ugonjwa huu katika kituo cha kutolea huduma za afya ili kuepuka kueneza maambukizi .

Tujitahidi kujilinda kwa magonjwa ya milipuko, na ukiona dalili zozote au kuna mtu ana dalili hizo muwahishe kwenye vituo vya huduma za afya.

Endelea Kusoma

Mfalme Salman wa Saudi Arabia aongoza kikao cha baraza la Mawaziri baada

Chaguo la Mhariri

Habari Mpya