Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema ataondoa wanajeshi wake nchini Niger mwisho mwa mwaka huu 2023 huku akiituhumu nchi hiyo kutokuwa tayari kupambana na ugaidi.
“Tunasitisha ushirikiano wetu wa kijeshi na mamlaka za Niger kwa sababu hawataki kupambana na ugaidi tena,” amesema Macron.
Macron amesema wanajeshi wa Ufaransa watarudi nchini kwao kwa utaratibu katika miezi ijayo huku akiweka wazi kuwa ni mwishoni mwa mwaka huu.
Macron ametoa kauli hiyo ikiwa ni wiki chache tangu Rais wa mpito wa Niger, Kanali Amadou Abdramane kumtaka Rais wa Ufaransa aondoe vikosi vyake vya jeshi pamoja na balozi wake nchini humo.
“Uwepo wa majeshi ya Ufaransa yanajumuisha uingiliaji wa wazi zaidi katika masuala ya ndani ya Niger, tunamtaka Rais wao ayaondoe haraka,” alisema Rais huyo wa mpito wa Niger aliyeingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi.