ZINAZOVUMA:

Tumuenzi Lowassa kwa kuiga mazuri yake – Mufti

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir ametoa...

Share na:

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir ametoa rai kwa watanzania kumuenzi Marehemu Mzee Edward Lowassa kwa kuiga mazuri aliyofanya wakati wa uhai wake, na kwamba kwa njia hiyo taifa litafaidika na mazuri yake.

Kiongozi huyo alitoa rai hiyo Februari 12, wakati alipofika Nyumbani kwa Mh. Lowassa kutoa pole kwa familia ya marhumu, ndugu, jamaa na marafiki wa kiongozi huyo aliyefariki Februari 10 wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Jijini Dar es salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukutana na familia pamoja na waombolezaji wengine, Sheikh Abubakar Zubeir amesema Lowassa aliwatumikia wananchi kwa moyo mkunjufu katika nafasi zake mbalimbali na kwamba wito alioutikia kutoka kwa mola wake ni wa watu wote.

“Kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislam Bakwata, nitumie fursa hii kuwapa pole wafiwa, pia nimpe pole Rais wa awamu ya sita wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa msiba huu mkubwa.”

“Msiba huu unagonga nyoyo za watanzania wengi kutokana na Mzee Lowassa alivyoweza kuishi na watanzania wenzake, lakini Mwenyezi Mungu ana mambo yake, matakwa yake, inafika wakati mtu kuitikia wito ni lazima.

Mzee wetu ameitwa na yeye ameitikia wito wa Mungu, hii ni njia ya kila mmoja wetu, dunia ni mahali pa kupita na sio pa kukaa. Sisi sote ni wa mwenyezi Mungu na Kwake Tutarejea,” alisema
Viongozi wamiminika msiba wa Lowassa.

Katika hatua nyingine, viongozi mbalimbali wa kitaifa walimiminika katika msiba wa Lowassa kwa lengo la kutoa pole kwa ndugu jamaa na marafiki.

Miongoni mwa waliofika msibani na kutoa pole kwa familia na watanzania kwa ujumla kutokana na msiba huo mkubwa nin Rais wa awamu ya nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete.

Akisimulia historia fupi na jinsi anavyo mfahamu Mh. Lowassa, Kikwete amesema wamekuwa pamoja tangu ujana mpaka wanakuwa viongozi.

Ameongeza kusema kuwa mchango wa Lowassa kwa taifa ni mkubwa.

“Nimepokea kwa mshituko taarifa ya kifo, nilikuwa nafahamu kwamba anaumwa lakini sikutegemea kwamba ingefikia hapa ilipofikia, ninamfahamu marehemu kwa muda mrefu tulikuwa Vijana pamoja, tulikuwa chuo Kikuu pamoja, tukatangulia sisi kuingia kwenye chama na baadaye yeye akafuata na tumefanya kazi pamoja kwenye chama kwa muda huo wote baadaye nikaendelea kwenye shughuli za jeshi mwenzangu akaendelea kwenye shughuli za chama, baadaye tukawa wabunge na tukafika Baraza la Mawaziri”

“Mwaka 1995 siku moja asubuhi nikapokea ugeni Mtoto akaja chumbani akaniambia Baba kuna ugeni nikawakuta marafiki zangu watatu, kaka yangu Samuel Sitta, Edward Lowassa na Rostam Aziz, wakaja kuniambia kwamba Msemaji Samuel Sitta kwamba tunataka muende na Edward Dodoma mkachukue fomu ya kugombea Urais Mimi nikasema jambo hilo halipo kwenye mawazo yangu, kama yeye lipo kwenye mawazo basi aende, naye akasema siendi bila ya wewe.”

“Basi tukabishana mpaka tukakubaliana kwamba wacha twende, tukaenda kuchukua fomu zile tukazijaza zikarudishwa, michakato ndani ya chama mwenzangu hakubahatika mimi nikabahatika kuwemo kati ya wale watano na baadaye tukapiga kura kwenye NEC nikawemo katika wale watatu, tukaenda mkutano mkuu nikawemo katika wawili lakini kura zangu hazikutosha akapata mzee Mkapa nikaja kuwa Waziri wake wa Mambo ya Nje na mwenzangu akaja kuwa waziri tena.”

“2005 tukajiandaa na Mimi nikapata nafasi ya kuchaguliwa kuwa Rais mwenzangu akaja kuwa Waziri Mkuu tukapata changamoto katikati mwenzangu ikabidi akae pembeni, tumeendelea kuwa Marafiki tukishirikiana kwa kila linalowezekana, ameugua Mwenyezi Mungu amechukua roho yake, ninachoshauri tu tuendelee kumuombea, Mungu aipokee roho yake aiweke mahali pema peponi, Edward ametoa mchango mkubwa katika Taifa letu, yaliyotokea ni changamoto katika maisha lakini hayafuti yale mema na mazuri aliyolifanyia taifa letu.”

Kwa upande wake Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), James ole Millya amesema marehemu Edward Lowassa alikuwa ni mtu mwenye urafiki wa kweli wakati wote.

Millya amesema Lowassa amefanya mengi katika uongozi wake, pia jamii yake ya wamasai nayo haita msahamu kwa mambo ambayo amekuwa akiwafanyia.

Alipambana kuwasaidia watoto wakike jamii ya wafugaji kusoma kwa bidii ili waje kuwa msaada mkubwa Kwa familia zao za kifugaji na jamii nyinginezo kwa ujumla.

“Mzee alikuwa ni mtu mwenye urafiki wa kweli bila unafiki, jamii imepoteza kiongozi ambaye itachukua muda kuziba pengo lake” alisema.

Mwili wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa unatarajiwa kuzikwa Februari 17, mwaka huu kijijini kwao Ngarash wilayani Monduli Mkoa wa Arusha.

Lowassa amefariki dunia Februari 10, 2024 saa 8 mchana katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Lowassa alifikishwa katika taasisi hiyo baada ya kuugua shinikizo la damu, matatizo ya mapafu na kujikunja kwa utumbo.

Ratiba ya mazishi imeanza Februari 13, 2024 na kuhusisha taratibu zote za kiserikali.

Endelea Kusoma

Vyombo vya Habari nchini Iran vimeanza kutangaza kifo cha Rais Ebrahim Raisi,