Chama cha watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wameitaka klabu ya Simba kuomba radhi kwa tukio waliloita la udhalilishaji.
Tukio hilo lilitokea Agosti 6, 2023 kwenye sherehe ya tamasha la siku ya Simba lililofanyika katika uwanja wa Taifa wa Benjamini Mkapa jijini hapa kwa kumpandisha mtu mwenye ulemavu wa ngozi akiwa amevishwa taulo ya watoto (baby diaper).
Akizungumza leo Jumatano Agosti 9, 2023 jijini Dar es Salaam mwenyekiti wa TAS, Godson Mollel amesema tukio hilo ni la pili kwa Simba kulifanya ambalo la kwanza lilikuwa Agosti 8, 2022 waliingia na jeneza ambalo lilimbeba mtu mwenye ualbino.
Amesema vitendo hivyo vinawatweza utu wa watu wenye ualbino nchini na kupelekea kuwepo kwa mijadala mingi katika jamii ikiwemo mitandaoni inaonyesha dhihaka kwa watu hao kinyume na haki za binadamu.
Mollel amesema kwa miaka mingi kumekuwa na jitihada kubwa za utetezi wa watu wenye ualbino nchini kutokana na historia ya madhila yaliyopelekea watu hao kupoteza maisha,pamoja na idadi kubwa ya wahanga wa vitendo vya ukatili na unyanyapaa.