Tanzania inatarajia kuwa nchi Mwenyeji wa Mkutano wa sita wa shirika la Usalama wa usafiri wa anga la Jumuiya ya Afrika Mashariki CASSOA. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Mei 15 na 16 mwaka huu visiwani Zanzibar.
Bw. Hamza Johari amesema kuwa mkutano wa CASSOA utakutanisha wadau wa kisekta na kujadili kwa kina mambo muhimu kuhusu usalama wa usafiri anga, pamoja na kutathmini athari za usafiri huo kwenye mabadiliko ya tabia nchi.
Bw. Johari ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania aliyasema hayo alipokuwa Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo utabebwa na kauli mbiu isemayo “kudumisha mifumo ya anga iliyo imara, endelevu, ya ubunifu, salama na yenye usalama” ikiwa na lengo la kuweka msisitizo katika usalama wa usafiri huo pamoja na ubunifu utakaosaidia kutunza mazingira Kwa mustakabali wa maendeleo endelevu duniani.
Aliongeza kusema kuwa wadau watakaohudhuria mkutano huo ni pamoja na Makampuni ya ndege, viwanja vya ndege, wasimamizi wa ndege na wadau wengine muhimu ambao watajikita katika Masuala yanayohusu usalama wa usafiri wa anga na mazingira.