Kiongozi wa kijeshi nchini Niger, Jenerali Abdourahamane Tchiani amesema jeshi lake halitatishwa na shinikizo za Kimataifa na kurejesha madaraka kwa rais Mohamed Bazoum lakini pia amelaani vikwazo alivyowekewa na ECOWAS.
Wakati Jenerali Tchiani akitoa kauli hiyo, Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, imetuma mjumbe kwenda kuzungumza na kiongozi huyo kurejesha mamlaka na kutahadharisha kuwa matumizi ya nguvu itakuwa ni hatua ya mwisho.
Katika hatua ya kuendelea kuliwekea jeshi la Niger shinikizo la kumrudisha Rais, Nigeria imekata umeme wake unaokwenda nchini Niger.
Hata hivyo kiongozi wa Jeshi la Niger Abdourahmane Tchani amesema “Vikwazo hivi ni vya kijinga na vya kidhalimu, vinalenga kudhalilisha majeshi ya ulinzi na usalama wa Niger, taifa la Niger na watu wake kwa lengo na kufanya nchi isitawalike kabisa.”