Serikali ya Senegal imepiga marufuku matumizi ya mtandao wa ‘Tiktok’ nchini humo katika kile ilichokiita ni hatua kuleta utulivu na usalama.
Waziri wa Habari na Mawasiliano amesema hayo siku chache baada ya kuweka vizuizi kwa huduma ya ‘internet’ huku maandamano yakiwa yanaendelea nchini humo.
Taarifa ya Waziri wa Habari na Mawasiliano inasema kwamba hatua ya kupiga marufuku ‘TikTok’T inatokana na mtandao huo kutumika na watu wenye nia mbaya ya kusambaza ujumbe wa chuki na wenye lengo la kutatiza usalama wa Senegal.
Huduma ya internet imezuiawa nchini Senegal tangu Jumatatu, na serikali imetumia hoja ya usalama na utulivu wa taifa hilo la Afrika Magharibi kutekeleza hatua hiyo.
Serikali imechukua hatua hizo baada ya kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko kufunguliwa mashtaka ya kupanga maandamano dhidi ya serikali, kupanga njama za uhalifu na makosa mengine mengi.
Senegal imekua ikishuhudia maandamano ya mara kwa mara na huku wanasiasa wa upinzani wakimshutumu Rais Macky Sall kumlimbikizia mashtaka ya uongo Sonko, ili kumzuia kugombea urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.