Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imejipanga kuwekeza katika rasilimali watu na fedha ili kuchochea maendeleo ya sekta ya viwanda ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Tamko la Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu uwekezaji huo lililotolewa jijini Dar Es Salaam mwezi Julai 2023.
Hayo yamebainishwa jijini Luanda, Angola na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax kwenye Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC ulioshirikisha nchi 16 wanachama wa jumuiya hiyo.
Dkt Tax alisema kuwa tamko la Dar Es Salaam limeainisha masuala mbalimbali ya utekelezaji kwa ajili ya kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu ambayo yameendelea kujadiliwa katika Mkutano wa 43 wa SADC ili kuhakikisha kuwa, katika kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu ambayo inahusu umuhimu wa rasilimali watu na fedha katika maendeleo endelevu ya viwanda, tamko la Dar Es Salaam linakuwa sehemu ya utekelezaji wa kaulimbiu hiyo.
“Suala la uwekezaji katika rasilimali watu, suala la uendelezaji wa rasilimali watu katika kuendeleza uchumi, ni vitu ambavyo tunaendelea kuvisukuma kama ilivyokuwa kwenye mkutano jijini Dar es Salaam ambapo Rais wetu alikuwa Mwenyekiti wa mkutano ulioangazia masuala ya rasilimali watu uliofanyika Tanzania”, alieleza Dkt. Tax