Kuanzia siku ya kesho Jumanne Afrika Kusini inatarajia kuanza kuwapokea wakuu wa nchi za Brazil, China, India, na mkuu wa diplomasia ya Urusi, pamoja na viongozi wengine wa nchi za kusini, wakiwemo viongozi zaidi ya thelathini kutoka Afrika .
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema katika moja ya masuala makuu yatakayokuwa kwenye ajenda ya mkutano huo wa 15 wa BRICS, ni kuhusu upanuzi wa kundi hilo, na uwezekano wa kutoa nafasi kwa nchi nyingine kujiunga.
“Zaidi ya nchi ishirini kutoka kote dunia wametuma maombi rasmi ya kujiunga na BRICS. Na Afrika Kusini inaunga mkono kuongeza wanachama” alisema Cyril Ramaphosa.
Aidha Rais Ramaphosa amesema kwa upande wao Kuwa mwanachama wa BRICS kumeleta matumaini na fursa kwa wananchi wa Afrika Kusini.
Akaongeza kuwa hilo limewezesha uchumi wa Afrika Kusini kuunda ushirikiano wa kimkakati na China, nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani.