Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza kuwa muungano wa BRICS utawasajili wanachama wapya sita mwanzoni mwa mwaka ujao.
Iran, Argentina, Misir, Ethiopia, Saudi Arabia na Milki ya falme za kiarabu zitakuwa nchi za kwanza miongoni mwa nchi nyingi na zilizotamani kujiunga na BRICS.
Mjadala wa kuhusu upanuzi wa muungano huo unaojumuisha nchi za Brazil, Urusi, India , China na Afrika kusini, umetawala agenda ya kikao kilichofanyika jijini Johannesburg.
Idadi kubwa ya mataifa yalikuwa yametuma maombi rasmi ya kujiunga na BRICS, ambayo inawakilisha robo ya uchumi wa dunia na zaidi ya watu bilioni tatu.
Baadhi ya wakuu wengine 50 wa nchi na serikali wamehudhuria mkutano huo mjini Johannesburg, ambao unakamilika siku ya Leo.