Wasaidizi wa Rais wa China, Xi Jinping jana Jumatano Agosti 23, 2023 wameripotiwa kuzuiwa kuingia katika ukumbi wa mkutano wa Brics unaofanyika jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Video fupi inayosambaa katika mitandao ya kijamii inaonyesha kuwa Xi Jinping alipokuwa akiingia ukumbini mtu anayedaiwa kuwa afisa wa usalama wa China alimfuata ili kuingia nae lakini alizuiwa mlangoni na maafisa wa usalama wa Afrika Kusini.
Ingawa kwa sasa haijulikani ni nini kilisababisha mkanganyiko huo, baadhi ya ripoti zimedokeza kwamba afisa huyo wa usalama alikuwa mtafsiri rasmi wa Rais Xi.
Mkutano wa Brics unahusisha Marais wa nchi wanachama ambazo ni Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini ambapo Rais wa Russia, Vladimir Putin kutokana na sababu za kiusalama amehudhuria mkutano huo kwa njia ya video.