Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi amesema kuwa mradi wa bonde la mto Msimbazi “Jangwani” unatarajiwa kuanza tarehe 15 Aprili 2024, ambao utasimamiwa na Wakala wa barabara za mijini na Vijiji TARURA.
Ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jijini Dar es salaam na kusema kuwa, mradi huo utaanza kwa kubomoa nyumba katika eneo la Jangwani kando kando ya mto Msimbazi.
Mobhare amesema wakazi hao walipewa wiki sita za kufanya utaratibu wa kuhama katika eneo hilo, huku akieleza kuwa fidia zao wameshalipwa na nyumba zote zinazotarajiwa kubomolewa zimeshawekewa alama.
Aidha amesema kimsingi wakati TARURA ikipanga mradi wa Jangwani, ilizingatia makubaliano na wamiliki wa majengo na nyumba hizo ambapo zilifanyiwa tathmini na kulipwa fidia.
“Hadi kufikia tarehe 26 Februari 2024, TARURA ilikuwa imeshaingiza malipo ya fidia ya kiasi cha shilingi Bilion 52. 61, kwenye account za wamiliki wa nyumba ambao walijiandikisha katika daftari la kwanza na sasa TARURA inakamilisha malipo kwa wengine waliosalia ambao walijiandikisha katika daftari la pili” amesema Msemaji Mkuu wa Serikali.