Nchi ya Iran imetangaza likizo ya siku mbili kwa wafanyakazi wa serikali na wale wa benki kutokana na hali ya ongezeko la joto nchini humo.
Uamuzi huo umetolewa wakati ambao dunia inakabiliwa ongezeko la joto la kihistoria na ambalo halijawahi kutokea.
Ofisi ya hali ya hewa ya Iran ilisema joto linaweza kuwa kati ya nyuzi joto 40 na 50 katika miji mingi ya nchi hiyo.
Katika Majimbo ya Ilam, Bushehr na Khuzestan, hivi karibuni kumerikoeiwa viwango vya joto zaidi ya nyuzi joto 45 kama ilivyoripotiwa na chombo cha habari cha Iran kinachomilikiwa na serikali, IRIB.
Kwa upande wa Dehloran, mji ulioko magharibi mwa Iran, ulirekodi joto la juu zaidi la nyuzi joto 50 katika muda wa saa 24 zilizopita.
Aidha Wizara ya Afya ya Iran imeendelea kutoa maonyo kuhusu kiharusi cha joto kutokana na kupigwa na jua kupita kiasi.