Bunge la Ghana limepiga kura ya kuondoa hukumu ya kunyongwa mpaka kufa na hivyo imeongeza idadi ya nchi za Afrika ambazo zimeondoa hukumu hiyo.
Mpaka sasa kulikuwa na wanaume 170 na wanawake sita waliokuwa wakisubiri kunyongwa nchini Ghana, ambao hukumu zao sasa zitabadilishwa na kuwa kifungo cha maisha.
Adhabu ya kifo nchini Ghana ilitekelezwa mara ya mwisho mwaka 1993.
Hukumu ya kifo kwa muda mrefu imekuwa kawaida nchini Ghana kwa watu waliopatikana na hatia ya mauaji.
Kura za maoni zimeonyesha kuwa raia wengi wa Ghana wanaunga mkono kukomeshwa kwa hukumu hiyo ya kunyongwa mpaka kufa.
Aidha miongoni mwa makosa ambayo hukumu yake huwa ni kunyongwa nchini Ghana ni pamoja na uhaini.