Watu watano ambao ni madereva bodaboda wamefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na lori lililofeli breki eneo la Dodoma Makulu jijini Dodoma usiku wa kuamkia leo.
Lori lilikuwa linatokea kwenye barabara inayotokea Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambapo lilifeli breki na kwenda kuparamia Kijiwe cha Bodaboda cha Amani kilichopo kando ya barabara hiyo na kusababisha maafa.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera amesema tukio hilo limetokea jana Desemba 11, 2025 saa 2:30 usiku ambapo katika ajali hiyo mtu mmoja alijeruhiwa ambaye ni utingo wa lori hilo.
Kamanda Hyera amesema athari nyingine iliyosababishwa na ajali hiyo ni uharibifu wa pikipiki za vijana hao pamoja na kuharibiwa kwa ukuta wa uzio wa nyumba iliyokuwa karibu na barabara ambao uligongwa na lori hilo.



