Benki ya dunia imetangaza kusitisha mikopo kwa nchi ya Uganda kutokana na nchi hiyo kupitisha sheria kali dhidi ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Benki hiyo imesema sheria hiyo inayoharamisha LGBTQ iliyopitishwa nchini humo inakwenda kinyume na misingi na maadili ya benki ya dunia ambayo haibagui yeyote kwa misingi ya jinsia, jinsi au rangi yake katika azma yake ya kutokomeza umasikini duniani.
Tangu kupitishwa kwa sheria hiyo inayotoa adhabu kali kwa wanaojihusisha na LGBTQ, nchi kadhaa ikiwemo Marekani na Umoja wa Mataifa umelaani utawala wa Uganda kwa kuridhia kupitishwa kwa sheria hiyo.
Uganda imekuwa na msimamo mkali na wa wazi dhidi ya mapenzi ya jinsi moja, ikiyataja mapenzi ya jinsi moja kama kinyume na maadili ya utamaduni wa Uganda.